Waziri Jafo ashiriki zoezi la usafi Dodoma

Waziri Jafo ashiriki zoezi la usafi Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akishiriki katika zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi katika Soko la Bonanza jijini Dodoma pamoja na wafanyabiashara katika soko hilo leo Julai 30, 2022 na kusisitiza agenda ya usafi wa mazingira kuwa endelevu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akibeba taka na kuzipeleka katika vyombo maalumu vya kuhifadhi taka mara baada ya kushiriki katika zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi katika Soko la Bonanza jijini Dodoma pamoja na wafanyabiashara katika soko hilo leo Julai 30, 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akisukuma mkokoteni uliobeba taka  kuelekea  katika vyombo maalumu vya kuhifadhi taka kabla ya kusafirishwa kwenda Dampo mara baada ya kushiriki katika zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi katika Soko la Bonanza jijini Dodoma pamoja na wafanyabiashara katika soko hilo leo Julai 30, 2022.
Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na wafanyabiashara katika Soko la Bonanza jijini Dodoma mara baada ya kukamilika kwa zoezi la usafi katika soko hilo leo tarehe 30 Julai 2022.

==================================================================

Akiwa sokoni hapo amezungumza na wafanyabiashara na kutoa rai kwao kudumisha kwa vitendo kampeni ya usafi na mazingira kwa ujumla.

“Ndugu zangu agenda ya mazingira ni endelevu sote yatupasa kuitekeleza kwa vitendo na uwe ni utamaduni wetu sote” Dkt. Jafo alisisitiza.

Pia, amewapongeza wafanyabiashara sokoni hapo, mabalozi wa mazingira na wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza kushiriki kufanya usafi wa mazingira

Amemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) ndani ya kipindi cha siku 14 kuhakikisha anafanya ukarabati wa mfumo wa maji taka katika soko hilo ili kuondoa adha inayowakumba wafanyabiashara kwa sasa.

“Ukarabati huu wa Mfumo wa maji taka katika eneo hili ufanyike mara moja, Mkurugenzi wa DUWASA asimamie kwa karibu utekelezaji wake” Alisisitiza Dkt. Jafo.

Aidha, Waziri Jafo alisema kuwa Serikali inatarajia kuzindua Kampeni ya usafi wa mazingira itakayofahamika kama ‘My Dustbin’ kwenye mitaa ya mbalimbali nchi nzima.

Alisema kampeni hiyo itasaidia kuweka mitaa katika hali ya usafi kwa kuwa kila mwananchi anatakiwa kutupa taka kwenye mapipa yaliyoyopo kwenye mitaa badala ya kutupa ovyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu wa Jiji la Dodoma Bw. Dickson Kimaro alisema wamekuwa wakihamasisha wananchi kushiriki usafi wa mazingira ili kuweka jiji katika hali ya usafi. Bw Kimaro alilisitiza uwajibikaji wa kila mwananchi katika kuhakikisha usafi unafanyika Mita tano kuzunguka maeneo ya Makazi  na Biashara. 

Alisema katika soko hilo wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wamekuwa wakijitokeza kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira sokoni hapo hivyo kuliweka jiji katika hali ya usafi.

Makamu wa Rais awasili mkoani Mbeya

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya Jacob Mwakasole pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali na chama na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama wakati alipowasili katika uwanja Ndege wa Kimataifa wa Songwe leo tarehe 30 Julai 2022 kwaajili ya ufunguzi wa maonesho ya nane nane yanayofanyika mkoani Mbeya kuanzia tarehe 1 Agosti 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifurahia muziki wa kwaya ya utumishi wa umma ya mkoa wa Mbeya wakati alipowasili katika uwanja Ndege wa Kimataifa wa Songwe leo tarehe 30 Julai 2022 kwaajili ya ufunguzi wa maonesho ya nane nane yanayofanyika mkoani Mbeya kuanzia tarehe 1 Agosti 2022.

==================================================================

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 30 Julai 2022 amewasili katika uwanja Ndege wa Kimataifa wa Songwe  mkoani Mbeya akitarajiwa kufanya ufunguzi wa maonesho ya Nane Nane yanayofanyika mkoani Mbeya kuanzia tarehe 1 Agosti 2022.

Katika Uwanja huo wa ndege Makamu wa Rais amepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya Jacob Mwakasole, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Waziri Kindamba, viongozi mbalimbali wa serikali na chama na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, wananchi mblimbali na kwaya 

ya utumishi wa umma ya mkoa wa Mbeya.

Dkt. Mpango aelekeza itolewe elimu kuhusu fursa za biashara ya hewa ya ukaa

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Katuma tarafa ya Mwese  Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi bilioni 2.3 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika na Vijiji nane vya Halmashauri hiyo kutoka katika mapato ya biashara ya hewa ukaa. Tarehe 23 Julai 2022.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika pamoja na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) namna wanavyohifadhi misitu pamoja na kupata mazao ya misitu wakati wa hafla ya kukabidhi hundi ya shilingi bilioni 2.3 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika na Vijiji nane vya Halmashauri hiyo kutoka katika mapato ya biashara ya hewa ukaa. Tarehe 23 Julai 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mheshimiwa Mwanamvua Mrindoko hundi ya shilingi bilioni 2 kwaajili ya vijiji nane vinavyotekeleza mradi wa uuzaji wa hewa ukaa vilivyopo tarafa ya Mwese wakati wa halfa iliofanyika Kijiji cha Katuma wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi leo taraehe 23 Julai 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mheshimiwa Mwanamvua Mrindoko hundi ya shilingi milioni 230 kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya uuzaji wa hewa ukaa  inayofanyika katika vijiji nane vya halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika.

====================================================================

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amemuagiza waziri mwenye dhamana ya mazingira kwa kushirikiana na watumishi kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi nchi nzima waweze kufahamu fursa zilizopo katika biashara ya hewa ukaa.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akikabidhi mfano wa hundi ya jumla ya shilingi bilioni 2.3 kwa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika pamoja na vijiji nane vya wilaya hiyo fedha zilizotokana na biashara ya hewa ukaa. Pia Ameitaka wizara kuhakikisha mapungufu ya kisera na usimamizi wa biashara ya hewa ukaa yanapatiwa ufumbuzi ili taifa liweze kunufaika na biashara hiyo.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa halmshauri zingine hapa nchini kujifunza kutoka Halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi namna ya kufaidika na biashara hiyo. Aidha ametoa wito kwa wizara ya maliasili na utalii kwa kushirikiana na serikali za mikoa kuwachukulia hatua kali za kisheria waharibifu wa mazingira ikiwemo wanaochoma moto misitu pamoja na  kusimamia sera na sheria ya mazingira ili kupunguza na kuondoa athari za kimazingira zinazoweza kujitokeza. Pia Makamu wa Rais ameagiza mkoa wa Katavi kufanya tathimini ya kimazingira na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa kushirikisha moja kwa moja jamii.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekemea vitendo vya wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi kwaajili ya shughuli za ufugaji na kilimo. Makamu wa Rais amewataka baadhi ya viongozi wa serikali na chama wanaruhusu wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi kuacha vitendo hivyo mara moja kwani vinahatarisha amani pamoja na kuchochea uharibifu wa mazingira.

Akitoa taarifa ya mradi wa hewa ukaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Shaban Juma amesema malengo ya mradi huo ni pamoja na kuhifadhi na kulinda misitu, bioanuai zote zilizo hatarini kutoweka wakiwemo sokwe mtu, kutunza vyanzo vya maji, kushirikisha jamii katika katika uhifadhi na kunufaika moja kwa moja na faida za uhifadhi. Ameongeza kwamba mradi unaiwezesha jamii kufanya shughuli za maendeleo ya vijiji kupitia mapato yatokanayo na uuzwaji wa hewa ukaa.

Mkurugenzi huyo amesema kupitia mradi huo halmshauri imekusanya zaidi ya milioni mia tatu tisini na nane ambazo zimesaidia katika uendeshaji wa halmashauri, utoaji wa bima za afya kwa wakazi wote waishio katika vijiji nane vya mradi huo, kujenga madarasa, kituo cha afya kata ya katuma pamoja na zahanati nne katika vijiji ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Biashara ya hewa ukaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ilianza mwaka 2018 ikiendeshwa na halamshauri hiyo na taasisi ya Carbon Tanzania kwa kushirikiana na mradi wa Tuungane kwa Afya na Mazingira bora. Jumla ya hekta 216,944 za misitu zimehifadhiwa katika vijiji nane vya tarafa ya Mwese na wananchi 34,242 wananufaika na biashara hiyo.

Awali Makamu wa Rais  Mhe. Dkt. Philip Mpango alisimama kuwasalimu wananchi wa Kijiji cha Ifukutwa kilichopo Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ambao walijitokeza barabarani kumlaki akiingiia katika Wilaya hiyo. Akiwa kijijini hapo, Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuharakisha ujenzi wa barabara ya kutoka Katavi kuelekea Uvinza Kigoma ili kuwasaidia wananchi shughuli za usafirishaji wa mazao pamoja na kufanya biashara kwa urahisi.

Aidha Makamu wa Rais amesisitiza suala la elimu kwa watoto wa Wilaya hiyo kwa kuwaasa wazazi na walezi kuhakikisha wanafuatlia maendeleo ya Watoto wao katika elimu pamoja na kusimamia wahitimu vema. Amesema mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya Watoto wa kike kushindwa kumaliza masomo kutokana na sababu mbalimbali kama ikiwemo ujauzito hivyo hakuna budi kupiga vita vitendo hivyo kwa nguvu zote. Pia Makamu wa Rais amewasihi kuzingatia lishe ili uzalishaji mkubwa wa chakula wanaoufanya uendane na afya zao.

Naibu Waziri Khamis awataka wavuvi kutunza mazingira

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khanis akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya boti sita za uvuvi na vifaa vyake iliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Shehia ya Jongoe Kisiwa cha Tumbatu Wilaya ya Kaskazini A Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar leo Julai 20, 2022.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akikabidhi boti sita za uvuvina vifaa vyake kwa kikundi cha wavuvi katika katika Shehia ya Jongoe Kisiwa cha Tumbatu Wilaya ya Kaskazini A Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar leo Julai 20, 2022 kupitia Mradi wa Kuhimili
Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akishiriki matukio mbalimbali wakati wa ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye alikabidhi boti sita za uvuvi kwa vikundi vya vya Shehia ya Jongoe Kisiwa cha
Tumbatu Wilaya ya Kaskazini A Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar leo Julai 20, 2022 kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwa katika boti kutokea Bandari ya Mkokotoni kuelekea Kisiwa cha Tumbatu kushiriki hafla ya makabidhiano ya boti sita za uvuvi kwa kikundi cha Shehia ya Jongoe leo Julai 20 kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu
wa Rais.
Sehemu ya boti sita za uvuvi na vifaa vyake vilivyokabidhiwa kwa kikundi cha wavuvi katika katika Shehia ya Jongoe Kisiwa cha Tumbatu Wilaya ya Kaskazini A Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar leo Julai 20, 2022 kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR)
unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

=================================================================

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza khamis ametoa rai kwa wanufaika wa mradi wa boti za uvuvi zilizotolewa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) kutofanya shughuli za kibinadamu zinazochangia

uharibifu wa mazingira.

Ametoa rai hiyo Julai 20, 2022 wakati wa hafla ya makabidhiano ya boti sita za uvuvi zilizokabidhiwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika Shehia ya Jongoe Kisiwa cha Tumbatu Wilaya ya Kaskazini A Mkoa wa Kaskazini Unguja,

Zanzibar.

Mhe. Chilo alisema boti hizo zitumike kuleta katika tija katika mapambano ya athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoikabili nchi yetu na duniani kwa ujumla, hivyo ni wajibu wa wanufaika wa mradi huo kuhakikisha wanatunza vyanzo vya maji, kufanya kilimo endelevu.

Alisema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inaendeleza ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na ndiyo maana inatekeleza miradi hii.

”Leo zinakabidhiwa boti hizi kwa vikundi vya wavuvi ambao ndio wanufaika wakuu kwa hiyo nitoe rai kwenu mtunze vyanzo vya maji ili viumbe vilivyomo navyo viweze kuishi kutunzwa na mazingira ndio kila kitu kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Chilo.

Aidha, Mradi wa EBARR ni wa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 na unatekelezwa katika Wilaya za Mvomero (Morogoro), Simanjiro (Manyara), Kishapu (Shinyanga), Mpwapwa (Dodoma) Tanzania Bara na Kaskazini A – Unguja, upande wa Zanzibar.

Maeneo ya Mradi yalichaguliwa kwa kuzingatia maeneo yenye ukame yenye jamii za wakulima, wafugaji, na wavuvi kwa lengo la kuongeza uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika jamii za vijijini kwa kuimarisha mifumo ikolojia na shughuli mbadala za kujiongezea kipato.