Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi akizungumza jambo wakati wa warsha ya mafunzo kwa maafisa wa Serikali waliopo katika Bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuhusu udhibiti wa uingizaji wa  kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal Jijini Dar Es Salaam.

Afisa Mfawidhi kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu Tanzania (TPHPA) Bw. Heri Mohamed akizungumza jambo wakati wa warsha ya mafunzo kwa maafisa wa Serikali waliopo katika Bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuhusu kuhusu udhibiti wa uingizaji wa  kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal, Jijini Dar Es Salaam.

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi akizungumza jambo na Maafisa Waandamizi kutoka Idara ya Uhamiaji, Mratibu Msaidizi wa Uhamiaji, Abel Ndijaraye na Mkaguzi wa Uhamiaji, Bi. Debora Kolongo wakati wa warsha ya mafunzo kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya itifaki ya montreal, Jijini Dar Es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa warsha ya mafunzo kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya itifaki ya montreal wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa wakati wa warsha hiyo ya Siku moja kwa Maafisa wa Serikali katika Bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Afisa Forodha kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. George Ngosso akizungumza akiwasilisha mada wakati wa warsha ya mafunzo kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya itifaki ya montreal, leo tarehe 15 Septemba, 2023 Jijini Dar Es Salaam.

Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Mitawi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha ya mafunzo kuhusu udhibiti wa uingizaji wa  kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal iliyofanyika Jijini Dar Es Salaam.

====================================================================

Serikali imewataka wasimamizi wa sheria katika maeneo ya Viwanja vya Ndege na Bandarini kuendelea na usimamizi na udhibiti wa kemikali zinazodhibitiwa kwa kuzingatia ukomo wa matumizi wa kemikali hizo.

Rai hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Mitawi wakati akifungua warsha kwa Maafisa wa serikali waliopo katika bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuhusu udhibiti wa uingizaji wa kemikali zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal.

Mitawi amesema Maafisa forodha na wasimamizi wa Sheria katika maeneo ya mipaka wana wajibu mkubwa wa kusimamia uingizaji wa bidhaa mbalimbali zinazoingizwa nchini zikiwemo kemikali ambazo zimekuwa zikileta madhara mbalimbali katika jamii yakiwemo magonjwa ya saratani ya ngozi, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na kujikunja kwa ngozi.

“Warsha hii ni muhimu kwenu na hii ni kutokana na majukumu yenu ya kila siku…. Naamini mtajenga uelewa mkubwa zaidi katika masuala ya Tabaka la Ozoni na hatimaye kuwa mabalozi wa kueneza elimu ya Ozoni kwa wengine ili sote kwa pamoja tuongeze juhudi za kuhifadhi Tabaka la Ozoni” amesema Mitawi.

Mitawi amesema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuepuka matumizi ya vifaa na kemikali ambazo zinasababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira ikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Mitawi amesema Maafisa wa Serikali na wasimamizi wa Sheria waliopo maeneo ya mipaka ni wadau muhimu katika udhibiti wa uingizaji wa bidhaa na kemikali zenye ukomo wa matumizi katika jamii na hivyo wana nafasi kubwa ya kuelimisha wananchi aina ya vifaa vinavyopaswa kutumika.

“Sote ni mashahidi…kuhusu athari za kiafya matumizi ya vifaa vyenye kemikali..Tumeshuhudia Serikali imekuwa ikitumia kiasi kikubwa cha fedha za matibabu kwa wagonjwa wa saratani na pia kumekuwepo na kiwango kikubwa cha joto siku hadi siku” amesema Mitawi.

Akifafanua zaidi Mitawi amesema nchi nyingi duniani kwa sasa zimeshuhudia athari za mabadiliko ya tabia ikiwemo hali ya ukame hatua inayosababisha hali ya ukosefu wa chakula katika maeneo mbalimbali Duniani, hivyo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuchukua hatua mahsusi kuhakikisha jamii ya Watanzania inabaki salama.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi Kemilembe Mutasa amesema katika kuelekea Siku ya Tabaka la Hifadhi ya Ozoni Tanzania imeendelea kupata mafanikio makubwa katika udhibiti wa kemikali zinazoharibu Tabaka la Ozoni.

“Tanzania sio mzalishaji wa kemikali hizi…Tumekuwa tukipokea kutoka nchi ya nchi..Tumeandaa kanuni, sera, sheria na miongozo mbalimbali katika…Tumekuwa na mfululizo wa mafunzo haya kwa watendaji wa Serikali kuwakumbusha wajibu wao katika maeneo yote ya udhibiti wa kemikali hizi” amesema Kemilembe.

Tarehe 16 Septemba kila mwaka, Tanzania huungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni . Kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka 2023 ni “Hifadhi ya tabaka la ozoni na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi”

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *