Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi (Advisory Board of the Global Centre on Adaptation – GCA).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa pongezi hizo jijini Dodoma leo Septemba 13, 2023 na kumtaja Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ni kiongozi wa mfano katika usimamizi wa mazingira hususan katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Jafo amesema kuwa kupitia Serikali anayoiongoza Tanzania imejipambanua katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ambayo ni chachu katika hifadhi ya mazingira.

Ametolea mfano wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) ambayo itatumia umeme na zaidi ya shilingi trilioni 23 zimetengwea kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo ambao utasaidia kupunguza gesi joto ambayo inachangia mabadiliko ya tabianchi.

Sambamba na hilo ametaja pia mradi wa mabasi wa mwendo kasi katika Jiji la Dar es Salaam umejipambanua, duniani sasa Tanzania imeaminika na kuwekewa mfano katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Uwekezaji katika Bwawa la Umeme la Nyerere ambapo zaidi ya shilingi trilioni 6.5 zimewekezwa ili kuja kuzalisha megawati 2,115 na miradi hii yote kimataifa inaonekana ni miradi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi,“ amesema.

Aidha, Dkt. Jafo amesema kuwa kazi kubwa ambayo Rais Dkt. Samia ameifanya katika kipindi cha miaka miwili ya uwekezaji katika Wizara ya kilimo kwa kuongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 294 hadi shilingi bilioni 950 na bajeti ya mwaka 2023/2024 imetengewa shilingi bilioni 970.

Amesema kazi zote hizo zinajionyesha namna Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyojipambanua katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi ndio maana dunia imeamua kumteua katika nafasi hiyo.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *