Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Ufunguzi wa katika Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024 linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Tarehe 27 Februari 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na viongozi mbalimbali wakati alipowasili katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kufungua Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024. Tarehe 27 Februari 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisikiliza maelezo kutoka kwa wadau wa sekta ya fedha wakati akikagua mabanda ya maonesho katika Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024 linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Tarehe 27 Februari 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwaongoza viongozi na washiriki mbalimbali wa Jukwaa la Kodi na Uwekezaji mwaka 2024 katika kuimba wimbo wa Taifa wakati wa ufunguzi wa Jukwaa hilo uliyofanyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Tarehe 27 Februari 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizindua Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024 linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Viongozi wengine ni Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Zena Said, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo. Tarehe 27 Februari 2024.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa wafanyabiashara mara baada ya kufungua Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa Mwaka 2024 linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Tarehe 27 Februari 2024.

=============================================================================

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya Awamu ya Sita, mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji yameimarika na kuwa bora zaidi kwa kipindi kifupi.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Ufunguzi wa Jukwaa la Kodi na Uwekezaji kwa mwaka 2024 lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam. Amesema Tanzania imeendelea kuwa kitovu cha uwekezaji na nchi yenye uchumi unaokua kwa kasi Kusini mwa Jangwa la Sahara licha ya misukosuko ya uchumi na kijamii inayoendelea Duniani kote. Ameongeza kwamba katika mwaka 2023, ukuaji wa Pato la Taifa unakadiriwa kuwa 5.0% ikilinganishwa na 4.7% mwaka 2022 huku matarajio kwa mwaka 2024 ni ukuaji wa 5.5%.

Makamu wa Rais amewasihi washiriki wa Jukwaa hilo kutoa maoni na mapendekezo kwa uhuru ili kuweza kuboresha vema sera za kodi na uwekezaji nchini. Amesema maoni yatakayotolewa katika Jukwaa hilo yatatumika katika mchakato wa Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025. Aidha  amewataka Mawaziri wa Fedha kuzingatia ushauri wa sekta binafsi na walipa kodi wote ili wadau waone umuhimu wa ushiriki wao katika jukwaa hilo. 

Halikadhalika ametoa wito kwa washiriki kujikita katika kuibua njia za kibunifu zitakazosaidia kuongeza mapato ya Serikali bila kuumiza Wafanyabiashara na Wawekezaji. Amewataka kujadiliana  kwa kina kuhusu namna ya kutumia  zaidi ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, mathalan kupitia hatifungani zitakazotolewa na taasisi na mashirika ya umma kugharamia miradi ya maendeleo.  Pia amewasihi mijadala kujielekeza katika kubaini na kudhibiti vihatarishi vya matumizi ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, ikiwemo wizi wa kimtandao na utoroshaji wa mitaji.

Makamu wa Rais amesema tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani imeendelea kufanyamaboresho ya sera, sheria na mifumo ya usimamizi wa kodi ili kujibu malalamiko ya Wawekezaji ikiwemo Kurekebisha sheria za kodi, Kuweka utulivu wa sera za kodi, Kuendelea kujenga na kuimarisha vituo jumuishi vya huduma za uwekezaji na biashara ikijumuisha ujenzi wa vituo 10 vya utoaji huduma kwa pamoja mipakani (One-Stop Border Posts), Kufanya mapitio na kuhuisha sera na sheria mbalimbali pamoja na Kukamilisha Mfumo wa Dirisha Moja la Kutoa Huduma kwa wawekezaji na wafanyabiashara kwa kuunganisha mifumo ya taasisi saba (7) ambazo ni NIDA, TRA, BRELA, TIC, Kazi, Uhamiaji na Ardhi.

Pia amesema hatua zingine zilizochukuliwa ni pamoja na Kuanzisha Ofisi ya Msuluhishi wa Malalamiko ya Walipakodi, kuwianisha majukumu ya kitaasisi ili kurahisisha utoaji huduma, Kuendelea kufanya mashauriano baina ya Serikali na sekta binafsi kupitia Baraza la Taifa la Biashara pamoja na kutoa vivutio vya kikodi ikiwemo kutoa misamaha ya kodi na kiwango cha asilimia sifuri (0) cha ushuru wa forodha kwa bidhaa mtaji na malighafi.

Makamu wa Rais amesema makusanyo ya mapato ya Serikali kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita yaliongezeka kwa 22.1% kutoka Sh. trilioni 17.6 mwaka 2020/21 hadi Sh. trilioni 22.6 mwaka 2022/23. Ongezeko hilo la ukusanyaji wa mapato limeiwezesha Serikali kuendelea kuongeza Bajeti yake kutoka Sh. trilioni 36 mwaka 2021/22 hadi Sh. trilioni 44.4 mwaka 2023/24.

Amesema Ongezeko la bajeti limewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa  (SGR) pamoja na injini na mabehewa yake, mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (94.8%, mradi wa Kinyerezi I Extension (100%) na mradi wa kufua Umeme wa Maji Rusumo (99.7%). Vilevile kupeleka huduma ya umeme kwenye vijiji 10,987 kati ya vijiji 12,318 vya Tanzania Bara (sawa na 89.19%), ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara na madaraja unaendelea ambapo jumla ya miradi 23 ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji ikiwa ni pamoja na daraja la Kigongo – Busisi (80.0%).

Kwa upande wake Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Wizara inatambua umuhimu wa kuongeza ushirikishwaji wa wadau kwa kuwa bado kuna changamoto katika masuala ya kujenga uchumi na kukuza ukusanyaji wa mapato ya ndani. Amesema bado ipo changamoto katika ulipaji wa kodi kwa hiari hasa matumizi ya mashine za kielektroniki na utoaji risiti.

Waziri Nchemba amesema bado ipo tabia ya kuwepo na visingizio mbalimbali vinavyopelekea kutotolewa kwa risiti za kielektroniki ikiwa ni pamoja na mnunuzi kuongozwa kukwepa kodi kwa kupewa bei ya chini ya bidhaa kutoka kwa muuzaji kwa sharti la kutopewa risiti. Amesema Jukwaa hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Rais ikikumbukwa utaratibu ambao umekuwa ukitumika siku zote ni kupata maoni ya wadau kupitia Vikao vya Kamati ya Maboresho ya Sera za Kodi. Ameongeza kwamba katika kuhakikisha wadau wengi zaidi wanashiriki kutoa maoni, Wizara iliandaa Jukwaa la Kodi lililofanyika tarehe 11 Januari 2023 jijini Dar es Salaam ili kupata maoni yao badala ya kuwasubiria kwenye vikao vya Kamati.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema tangu mwaka 2019 – 2023 Serikali imefanya mabadiliko na maboresho ya kisera, kisheria na kikanuni 665 yanayohusu kodi na yasiyohusu kodi. Amesema kati ya hayo maboresho 416 yamelenga kuweka mazingira bora ya biashara na uwekezaji nchini huku maboresho 460 yakiwa yamefanyika katika kipindi cha miaka 3 iliyopita. 

Ameongeza kwamba kwa sasa Tanzania inakidhi vigezo vikubwa vya mazingira bora ya uwekezaji ikiwemo vigezo vya kuwa na utulivu wa kisiasa na amani, mazingira bora ya kisheria na urekebu, uwepo wa soko la bidhaa zitakazozalishwa,utulivu wa kiuchumi, vipaji na nguvukazi, ubora wa miundombinu, viwango vya chini vya kodi, uwepo wa ardhi pamoja na uwepo wa fedha za kugharamia miradi ya uwekezaji wa ndani. 

Kauli Mbiu ya Jukwaa la Kodi na Uwekezaji mwaka 2024 ni “Maboresho ya sera katika uwekezaji, ukusanyaji wa mapato ya ndani na ukuaji wa uchumi jumuishi”. Jukwaa hilo linafanyika tarehe 27-28 Februari 2024 likiwakutanisha wadau mbalimbali.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *