Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo akizungumza wakati akifungua semina kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma walio chini ya Klabu ya Kupinga Rushwa (UDOSOAC) iliyofanyika jijini Dodoma leo Julai 20, 2021.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Faustine Karrani Bee akitoa neno la ukaribisho wakati wa akifungua semina kwa wanafunzi wa Chuo hicho walio chini ya Klabu ya Kupinga Rushwa (UDOSOAC) iliyofanyika jijini Dodoma leo Julai 20, 2021.
Sehemu ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wakiwa katika semina Mapambano dhidi ya Rushwa iliyofanyika jijini Dodoma leo Julai 20, 2021.
———————————————————————————————————————————-

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo amesema rushwa ni saratani kubwa inayokwamisha maendeleo kwa wananchi.

Jafo amesema hayo leo Julai 20, 2021 wakati akifungua semina kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma walio chini ya Klabu ya Kupinga Rushwa (UDOSOAC) iliyofanyika jijini Dodoma.

Alisema kuwa vitendo vya rushwa vinasababisha wananchi washindwe kupata huduma za kijamii na hivyo kuchangia ukiukaji wa haki za msingi wanazostahili kuzipata.

Waziri Jafo aliongeza kuwa Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kwa wananchi lakini zinaingiliwa na vitendo vya rushwa hali inayosababisha ijengewe chini ya kiwango.

“Ndugu zangu leo hii mkandarasi akipewa dhamana ya kujenga barabara ya kilomita 10 na upana wa mita 7. 5 na kwa vile kuna mazingira ya rushwa msimamizi wa mradi yuko site atashindwa kumsimamia mkandarasi huyo na atajenga chini ya kiwango,” alisema.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha UDOM, Prof. Faustine Karrani Bee alitoa rai kwa kila mwananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa ili wahusika wachukuliwe hatua.

Alisema rushwa ya ngono ni changamoto kubwa katika vyuo hapa nchini na kuongeza kuwa mapambano dhidi ya vitendo hivyo yameshirikisha vijana wa vyuo kwa kuwa ndio wanakumbana navyo.

“Nawaomba vijana wote acheni kabisa kujihusisha na vitendo hivi vya rushwa, kataeni kupokea au kutoa rushwa kwani tunataka vyuo vyetu visonge mbele,” alisisitiza.

Semina hiyo ilitolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kupitia kwa Kamanda wa Taasisi hiyo Mkoa wa  Dodoma, Bw. Sosthenes Kibwengo.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *