Serikali yachukua hatua kudhibiti uharibifu wa mazingira ya baharini

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zimekuwa zikichukua juhudi za kisera, kisheria na kuandaa miongozo ya utunzaji wa mazingira ya baharini ili kuhakikisha uharibifu unadhibitiwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo Aprili 12, 2022.

Mbunge wa Wete Mhe. Omar Ali Omar alitaka kujua namna Serikali ilivyojipanga kukabiliana na uharibifu unaotokana na ukataji mikoko na uvunaji wa matumbawe ili kuvinusuru visiwa hivi visitoweke katika uso wa dunia.

Naibu Waziri Khamis alisema katika kukabiliana na changamoto hizo miongoni mwa juhudi zinazofanyika ni kujenga uelewa kwa wanajamii juu ya utunzaji wa mazingira na rasilimali za bahari ikiwemo uhifadhi wa mikoko na matumbawe.

Alisema kuwa pamoja na juhudi hizo pia kunafanyika upandaji wa mikoko na matumbawe katika maeneo yaliyoathirika kwa kutumia njia mbalimbali endelevu na za kitaalamu.

Alibainisha kuwa hekta 7 za mikoko zimepandwa Unguja na hekta 10 zimepandwa Pemba katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2021 pamoja na kuweka matumbawe bandia 90 Unguja na Pemba aina ya reef ball yalipandikizwa katika kijiji cha Jambiani na mapande maalum Layer Cakes 6 katika kijiji cha Kukuu.

Mhe. Khamis alisema Serikali imeshirikisha jamii katika kusimamia maeneo ya mikoko na matumbawe ikiwemo kuanzisha hifadhi ndogo ndogo za kijamii katika maeneo ya Kukuu, Fundo, Makoongwe kwa kisiwa cha Pemba na maeneo ya Mtende, Tumbatu na Kizimkazi kwa kisiwa cha Unguja.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *