Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akisikiliza maelezo kuhusu ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Kijiji cha Lukenge wilayani Mvomero mkoani Morogoro unaotekelezwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akikagua ujenzi wa tangi la majisafi katika Mingo wilayani Mvomero mkoani Morogoro unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR).

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akisaini kitabu alipowasili wilayani Mvomero mkoani Morogoro kwa ajili ya ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR).

Sehemu ya mfereji wa skimu ya umwagiliaji Kijiji cha Lukenge wilayani Mvomero unaojengwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) ambao Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo aliukagua na kutoa maelekezo.
====================================================================

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameelekeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuunda timu kukagua kusuasua kwa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Lukenge wilayani Mvomero na kuwasilisha taarifa ndani ya mwezi mmoja.

Amechukua hatua hiyo tarehe 17 Juni, 2022 wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwa ajili ya kutembelea na kukagua Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.

Dk. Jafo alionesha kushangazwa na hali aliyoikuta katika mradi huo unaosimamiwa na wataalamu kutoka Wilaya ya Mvomero wakati Serikali ilishatoa fedha zote ili utekelezaji huo ufanyike kwa wakati kama ilivyopangwa.

“Nimekuja kuangalia value for money, sijaridhishwa na mwenendo wa usimamizi wa mradi huu wataalamu wametuingiza chaka hatuwezi kuvumulia wataalamu wachache wanaotuvuruga, kwa hiyo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na ndani yake wakiwemo TAKUKURU wachunguze mradi huu, tunataka kuona mradi huu unakamilika kwa wakati tufanye kazi kwa maslahi ya wananchi,” alisema.

Hata hivyo, kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa EBARR wilayani humo, Bw. Baraka Mteri alisema mradi huo ulianza kujengwa mwaka 2013/14 umekaa kwa zaidi ya miaka tisa bila kuendelezwa hivyo waliwasilisha ombi hilo Ofisi ya Makamu wa Rais ambayo ilikubali kutoa fedha kiasi cha sh. milioni 710.

Alisema baada ya kupata fedha Mkurugenzi wa Wilaya alituma wataalamu wakague eneo hilo walibaini changamoto kuwa liko usawa wa chini ukilinganisha na usawa wa mashamba.

“Wananchi wana kiu kuona mradi huu ukikamilika kwa wakati ili uwasaidie kupata majawabu ya mustakabali wa maisha yao sasa hapa tunataka mradi huu iwe mvua iwe jua tutaka uanze kufanya kazi,” alisisitiza.

Aliitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ijipange kununua pampu ya kusukuma maji kwa kuwa wao ndio wasanifu wa mradi huo ili uweze kuanza kufanya kazi kama ilivyotarajiwa.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo alitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kisima cha maji safi katika Kijiji cha Mingo wilayani humo ambapo alioneshwa kuridhishwa na utekelezaji wake.

Alitoa maelekezo kwa wataalamu kutoka Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) kukamilisha mradi huo Juni 28, 2022 kama walivyomuahidi ili uweze kusaidia wananchi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Nataka nione maji yanatiririka hapa na kwenda kwa wananchi itakapofika asubuhi ya tarehe 29 mwezi Juni, tunataka kuona wananchi wanafaidika na miradi hii ya mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais,” alisema.

Akiishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mingo, Bw. Rashid Kibukila aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwapelekea mradi huo.

Mbali ya Mvomero, mradi wa EBARR pia unatekelezwa katika halmashauri za wilaya za Mpwapwa (Dodoma), Kishapu (Shinyanga), Simanjiro (Manyara) na Kaskazini ‘A’ (Unguja).

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *