Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na viongozi mbalimbali wa dini mara baada ya kuhitimishwa kwa Dua na Maombi ya kuliombea Taifa kuelekea Miaka 60 ya Muungano yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma tarehe 22 Aprili 2024.

=============================================================================

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameungana na viongozi wa dini pamoja na watanzania kwa ujumla katika Dua na Maombi kwaajili ya kuliombea Taifa kuelekea Miaka 60 ya Muungano, Dua na Maombi hayo yamefanyika katika Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma leo tarehe 22 Aprili 2024.

Akihutubia mara baada ya maombi na dua ya kuliombea Taifa, Makamu wa Rais amesema Katika kipindi cha miaka 60 ya uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Taifa limeendelea kupiga hatua katika sekta mbalimbali na hivyo kuendelea kuboresha maisha ya Watanzania.

Amesema tangu Muungano ulipoasisiwa mwaka 1964 umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka ambapo changamoto mbalimbali za Muungano zimekuwa zikitatuliwa kupitia mazungumzo ya pamoja na hivyo kujenga maelewano na mshikamano katika Taifa. Amesema mafanikio hayo ni kutokana na udugu na ushirikiano wa wananchi wa pande zote mbili za Muungano uliokuwepo tangu zamani na nia ya dhati ya kujenga nchi na jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani. Amewasihi wananchi kuendelea kuenzi na kudumisha tunu za Taifa ambazo ni amani, umoja, mshikamano, utu, haki, heshima ya mwanadamu, uhuru na demokrasia.

Aidha Makamu wa Rais amesema wakati ikitimia miaka 60 ya Muungano, bado ni muhimu kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza kasi ya maendeleo, kukuza ustawi wa jamii na kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili Taifa. Halikadhalika amewasihi watanzania wote kwa pamoja kwa kuongozwa na viongozi wa dini, Serikali, wazazi, walezi na walimu kuwajibika kuendelea kukabiliana na mmomonyoko wa maadili katika Taifa unaopelekea kuongezeka kwa matendo yanayokiuka mila na desturi za Kitanzania ikiwemo uhalifu, ukatili, matumizi ya dawa za kulevya na mengineyo ambayo hayampendezi Mwenyezi Mungu.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amesema serikali itaendelea kuchukua hatua katika kudhibiti uhalifu na ufujaji wa fedha za umma. Amewataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo husika pale uovu unapofanyika katika jamii ili hatua ziweze kuchukuliwa. Ametoa wito kwa Mihimili yote kufanya kazi kwa ushirikiano kwa manufaa ya nchi na watu wake. Amewasihi Watanzania kutumikia nchi kwa haki uadilifu na uzalendo.

Vilevile Makamu wa Rais amesema Serikali inatambua na kuthamini ushirikiano mzuri uliopo baina yake na Taasisi za dini nchini na itaendeleza ushirikiano huo kwa manufaa na ustawi wa Taifa. Amewashukuru viongozi wote wa dini nchini kwa kuendelea kuliombea Taifa pamoja na kuendelea kukemea maovu, kuonya, kufundisha maadili mema na kutoa huduma za kiroho na kijamii kwa Watanzania. Aidha, amewapongeza Viongozi wa Dini kwa mchango mkubwa katika kuhakikisha Watanzania wanaendelea kubaki wamoja na kuendelea kushirikiana licha ya tofauti za dini, kabila, rangi, ufuasi vyama vya siasa au mahali wanapotoka.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema vijana wa sasa wana kisa sababu kuhakikisha wanaulinda, kuusimamia, kuimarisha na kutetea muungano ili uendelee kudumu daima na vizazi vijavyo viukute Muungano ukiwa salama na wenye mafanikio makubwa.

Amesema Muungano unadumisha umoja, amani, mshikamano na upendo na kutoa uhuru kwa wananchi wa pande zote mbili kuweza kufanya shughuli za kijamii na kiuchumi.

Dua na Maombi hayo yameongozwa na viongozi wa dini pamoja na kujumuisha waumini, waimbaji wa muziki wa dini wa kikristo na kiislamu. Aidha maombi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma, Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais (Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi) Hamza Hassan Juma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, Wabunge pamoja wananchi mbalimbali.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *