Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Masauni Yussuf Masauni amesema kuwa Serikali ya Tanzania imechukua hatua za kuimarisha uhifadhi wa maeneo ya bahari yaliyohifadhiwa.
Amesema hatua hizo zimesaidia kukuza usimamizi endelevu wa uvuvi na kuongeza uwezo wa kuzuia uchafuzi wa baharini na kukabiliana na hatari za mabadiliko ya tabianchi.
Mhandisi Masauni amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Kwanza wa Kamati Tendaji ya Mkataba wa Nairobi kuhusu Hifadhi, Usimamizi na Uendelezaji wa Mazingira ya Bahari ikiwa ni baada ya Mkutano Mkuu wa 11 wa nchi Wanachama uliofanyika nchini Madagascar Agosti, 2024.
Mkutano huo umefanyika jijini Dar es Salaam leo Januari 30, 2025. Ameeleza kuwa eneo la Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi lina mifumo mbalimbali ya ikolojia ya pwani na baharini ambayo inasaidia kukuza uchumi na hivyo ni muhimu kuwa na usimamizi endelevu wa mazingira yake.
Mhe. Masauni ametaja ukanda huo kuweza kutoa huduma muhimu za mfumo ikolojia ikiwemo hifadhi ya bioanuwai ya baharini ambayo inachukuliwa kuwa moja ya mifumo ikolojia yenye thamani zaidi ulimwenguni ambayo ina manufaa makubwa kwa jamii za pwani.
Ameshukuru na kupongeza Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kupitia Sekretarieti ya Mkataba wa Nairobi kwa kusimamia ajenda ya uhifadhi wa mazingira ya bahari kupitia ufadhili wa miradi yenye lengo la kuboresha maisha ya jamii za wavuvi hususan katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, Tanzania.
Halikadhalika, ametoa shukrani kwa UNEP kwa kuipatia Serikali ya Tanzania takribani dola za kimarekani 70,000 kwa ajili ya kukamilisha Mradi wa Upanuzi wa Kituo cha Kutibu Majitaka cha Msingini huko Chake Chake, Pemba.
Ameongeza kuwa eneo la pwani ya Tanzania lina rasilimali nyingi za baharini ambazo ni pamoja na fukwe za mchanga, miamba, mito, misitu ya mikoko, nyasi bahari na matumbawe.
Sanjari na hilo, Mhe. Masauni amesema kuwa mazingira ya bahari ya Tanzania yanasaidia aina mbalimbali za samaki wakiwemo papa, kasa na wengineo na miti ya mikoko ambayo inasaidia katika utunzaji wa mazingira.
“Pamoja na faida hiyo kubwa, kama nchi wanachama tunapaswa kutambua na kukabiliana na changamoto zinazokabili mazingira ya bahari na pwani zikiwemo mabadiliko ya tabianchi, uvuvi usio endelevu, uchafuzi wa mazingira na upotevu wa viumbe hai, jambo ambalo linatishia afya na ustahimilivu wa mifumo ikolojia,” amesema.
Nchi zilizozhiriki mkutano huo chini ya uenyekeiti wa Tanzania ni Comoro, Kenya, Mauritius, Msumbiji, Madagascar, Shelisheli, Somalia, Reunion ( Ufaransa) na Afrika Kusini