
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda mazingira, kuhifadhi misitu na kuboresha afya za wananchi.
Kwa sasa, asilimia 28.5 ya kaya na taasisi nchini zinatumia nishati safi ya kupikia, huku Serikali ikiwa na lengo la kufikisha matumizi hayo kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2034 na asilimia 100 ifikapo mwaka 2050.
Akizungumza katika Kongamano na Mdahalo wa Nishati Safi ya Kupikia, ulioandaliwa na Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) Zanzibar, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema Serikali inaendelea kuweka msukumo mkubwa katika matumizi ya nishati safi, huku kipaumbele kikitolewa kwa taasisi zinazohudumia na kulisha watu wengi, zikiwemo shule, magereza na kambi za mafunzo.
Dkt. Muyungi, ambaye aliongoza mjadala huo, amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kuongoza katika mpito kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo magereza yote nchini yamehamia katika matumizi ya nishati safi. Hatua hiyo inasaidia kupunguza matumizi ya kuni na hivyo kupunguza shinikizo na uharibifu wa misitu katika maeneo yenye magereza.
Aidha, Dkt. Muyungi ameipongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kampeni ya kusambaza majiko na mitungi ya gesi kwa wananchi wa maeneo ya vijijini, pamoja na TANESCO kwa mpango wa kukopesha wananchi majiko ya umeme yenye matumizi madogo ya nishati.
Kongamano na mdahalo huo uliofanyika Zanzibar tarehe 11 Agosti 2026 umeandaliwa na Mwanamke Initiatives Foundation (MIF) na kuwakutanisha wadau mbalimbali kujadili hatua, fursa na mikakati ya kuharakisha mpito kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha nishati safi ya kupikia inakuwa nafuu, salama na kufikiwa na wananchi wengi zaidi, ili kufanikisha malengo ya kitaifa ya kulinda afya za wananchi na kuhifadhi mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.