
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa akipanda mti katika siku ya usafi wa mazingira iliyoambatana na zoezi la upandaji miti wilayani Kondoa mkoani Dodoma.




=============================================================================================================
Ili kutekeleza Dira ya Taifa 2050 katika eneo la uhifadhi wa mazingira linalolenga kupanda zaidi ya miti bilioni mbili, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri zote 184 nchini kuanzisha vitalu vya miche ya miti.
Kwagilwa ametoa maelekezo hayo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Masauni alipomwakilisha katika siku ya usafi wa mazingira iliyoambatana na zoezi la upandaji miti wilayani Kondoa.
“Hatuwezi kufikia lengo la miti bilioni mbili tusipokuwa na utaratibu usioeleweka haiwezekani kwenye Halmashauri zetu za mikoa yote 26 mkaniambia mnapanda miti kila mwaka nikiwauliza vitalu vyeni viko wapi hamuwezi kunionyesha wenzetu wa TFS wanavyo vitalu vyao sasa haya ni maelekezo na vitalu hivyo visiishie kwenye ngazi ya Halmashauri viende kenye ngazi ya kata kwa kufanya hivyo ndio tutaweza kuvifikia vijiji vyetu,vitongoji vyetu, mitaa yetu pamoja na maeneo yote” amesema Mhe. Reuben Kwagilwa.
Amesema kuanzishwa kwa vitalu vya miche ya miti kuanzia ngazi ya Halmashauri hadi kata kutasaidia kuongeza upatikanaji wa miche na kurahisisha utekelezaji wa mpango wa upandaji miti katika vijiji, vitongoji, mitaa na maeneo mengine nchini.