Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu Rasmi ya Ofisi ya Makamu wa Rais

Tanzania, JICA zajadili ushirikiano usimamizi taka ngumu Dar
Nov 04, 2026
Tanzania, JICA zajadili ushirikiano usimamizi taka ngumu Dar
Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi (kulia) akifanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kujadili uwezekano wa ushirikiano katika kuboresha sekta ya usimamizi wa taka ngumu jijini Dar es Salaam ofisini kwake Mtumba jIjini Dodoma leo Novemba 04, 2026.
Na Robert Hokororo

Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi akizungumza na Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kujadili uwezekano wa ushirikiano katika kuboresha sekta ya usimamizi wa taka ngumu jijini Dar es Salaam ofisini kwake Mtumba jIjini Dodoma leo Novemba 04, 2026.

====================================================================================================================

Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kujadili uwezekano wa ushirikiano katika kuboresha sekta ya usimamizi wa taka ngumu jijini Dar es Salaam.

 

Kikao hicho kimefanyika Novemba 4, 2026, Ofisini kwake, Mtumba jijini Dodoma, huku Ujumbe wa JICA ukiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Afrika Mashariki, Idara ya Afrika, Bi. Mai Tomori aliyeambatana na Bw. Tadaya Yamamoto, Mshauri Mwandamizi kutoka Idara ya Mazingira ya Kimataifa, na Bi. Marika Tsugawa Afisa Mradi kutoka Idara ya Miradi ya Ruzuku.

 

Lengo la ziara ya Ujumbe huo ni kujadili uwezekano wa JICA kuchangia katika kuimarisha sekta ya usimamizi wa taka, hususan kuboresha mifumo na huduma za usimamizi wa taka ngumu katika Jiji la Dar es Salaam.

 

Ziara hiyo ni sehemu ya utafiti wa awali (Preparatory Survey) unaolenga kutathmini mahitaji na fursa za utekelezaji wa mradi unaopendekezwa. Utafiti huo unahusisha mashauriano na mamlaka za Serikali na taasisi zinazohusika na utekelezaji, kutembelea maeneo husika, kukusanya takwimu na taarifa muhimu, pamoja na kutathmini uwezekano wa mradi kwa kuzingatia masuala ya kiufundi, kifedha, kimazingira na kitaasisi.

 

Katika majadiliano hayo, pande zote mbili zilipata fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu changamoto na mahitaji yaliyopo katika usimamizi wa taka ngumu jijini Dar es Salaam, maeneo yanayoweza kupewa kipaumbele katika ushirikiano huo na hatua zinazofuata katika mchakato wa maandalizi ya mradi.

 

Ushirikiano huo unalenga kuweka msingi wa kuboresha huduma za usimamizi wa taka ngumu na kuimarisha juhudi za kulinda mazingira na kuboresha usafi wa Jiji la Dar es Salaam.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi

slot gacor