
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (katikati) akiwasili Shule ya Sekondari Arusha kuongoza zoezi la upandaji miti pamoja na kukagua mifumo ya nishati safi ya kupikia iliyopo shuleni hapo, Mei 22, 2026.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Joseph Mkude mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya kushiriki shughuli za utunzaji wa mazingira, Mei 22, 2026.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akisalimiana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Toba Nguvila mara baada ya kuwasili Shule ya Sekondari Arusha kwa ajili kuongoza zoezi kupoanda miti pamoja na kukagua mifumo ya Nishati Safi.

Naibu Katibu Mkuu (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda akisalimia na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Toba Nguvila mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ajili ya kushiriki shughuli mbalimbali za utunzaji wa mazingira, Mei 22, 2026.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akiongoza zoezi la usafi Kituo Kikuu cha Mabasi Mkoa wa Arusha, Mei 22, 2026.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akimkabidhi jiko la gesi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Arusha, Lorna Nteles ikiwa moja ya pongezi kwa shule hiyo kuwa mfano wa taasisi zinazotumia nishati safi ya kupikia.
===============================================================================================================
Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajiwa kuzindua Programu ya Kitaifa ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania katika kilele cha Siku ya Mazingira Duniani (WED) ambapo kitaifa itafanyika jijini Dodoma, Juni 5, 2026.
Akizungumza katika uzinduzi wa usafi wa Mazingira kuelekea siku hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni alisema lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya mfano duniani katika suala la Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira.
Alisema Programu hiyo inalenga kutekeleza Dira, 2050 hususan nguzo ya tatu kuhusu Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi ikiwa na lengo la kupanda miti bilioni 2 kwa mwaka, kuimarisha Biashara ya Kaboni, Uanzishaji wa Bustani za Kijani katika Miji na shughuli zingine za Kijani.
“Pia program hii inatarajia kuongeza ajira zinazoweza kufikia zaidi ya elfu ishirini na tano (25,000) ifikapo 2030 kupitia sekta za taka, misitu, kaboni na nishati safi,”alisema Mhe. Masauni.
Alifafanua kuwa tukio hilo ni sehemu ya juhudi za Kitaifa na Kimataifa za kulinda mazingira, kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga jamii yenye afya na ustahimilivu.
Aidha, alileza Dira, 2050 imeweka maono ya Taifa kuwa hadi kufikia mwaka 2050 Tanzania iwe kinara katika matumizi endelevu ya rasilimali, Taifa linalotumia taka kama malighafi kwa manufaa ya kiuchumi na Taifa kinara katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha ustahimilivu na uendelevu wa mazingira.
“Juhudi zinahitajika ili kutekeleza shughuli za mazingira kwa njia jumuishi inayohusisha makundi yote ya kijamii bila kujali jinsia au umri. Kwa jiji la Arusha, tafiti za mwaka 2020 zinaonesha kuwa jiji linazalisha takribani tani 550 za taka ngumu kwa siku, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya taka hizo zinaweza kurejelezwa ikiwa zitadhibitiwa vizuri kupitia uchumi rejeshi,"aliongeza.
"Kwa ngazi ya Kitaifa, Tanzania inakadiriwa kupoteza takribani hekta 469,420 za misitu kila mwaka kutokana na shughuli mbalimbali zisizo endelevu ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa ya kuni na mkaa, kilimo kisicho endelevu, ufugaji holela pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu zinazosababisha uharibifu wa mazingira hali inayochangia kuongezeka kwa gesi joto, kuharibu vyanzo vya maji na kuhatarisha usalama wa bioanuwai,".
Alieleza Upandaji wa miti yenye matumizi mbalimbali una mchango mkubwa katika kufyonza gesi ya kaboni, kupunguza mmomonyoko wa udongo, kuhifadhi vyanzo vya maji, kutoa matunda pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi kupitia bishara ya Kaboni na kuongeza ustahimilivu dhidi ya athari za Mabadiliko ya Tabianchi.