Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu Rasmi ya Ofisi ya Makamu wa Rais

Kamati ya Bunge yapongeza Miradi ya Muungano Zanzibar
Feb 19, 2025
Kamati ya Bunge yapongeza Miradi ya Muungano Zanzibar
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Florent Kyombo akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua Taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar leo Februari 19, 2025. Kushoto ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja.
Na Robert Hokororo

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imetoa pongezi kwa Serikali kwa kutekeleza na kusimamia miradi ya Muungano Zanzibar na hivyo kuleta manufaa kwa wananchi.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Florent Kyombo wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua Taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar leo Februari 19, 2025.

Miongoni mwa Taasisi zilizotembelewa na Kamati ni pamja na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC).

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara hiyo, Mhe. Kyombo amesema miradi hii ni matunda ya uongozi imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

Katika mradi wa Mbweni katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Karume (KIST) uliopo Mkoa wa Mjini Magharibi, Makamu Mwenyekiti amesema Kamati imeridhishwa na mradi huo.

“Tuwapongeze na kuwashukuru viongozi wakuu wa Serikali zote mbili kwani kupitia miradi hii, viongozi hawa wamefanya mapinduzi makubwa katika ujenzi wa miundmbinu na huduma za jamii na ubora wake unaonedkana,” amesema.

Mhe. Kyombo ambaye pia ni Mbunge wa Nkenge amewataka wananchi kuendelea kuwapa ushirikiano Viongozi hao wakuu na Serikali kwa ujumla ili miradi hiyo iwafikie na kutoa huduma stahiki.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Ofisi hiyo inatarajia kujenga jengo mahsusi litkalojumuisha taasisi zote za Muungano upande wa Zanzibar.

Amesema pamoja na mpango tayari Serikali ya Jamhuri ya Muungano imekwishajenga majengo ya taasisi zake ambayo yanaendelea kutoa huduma kwa wananchi.

“Niwaambie tu Serikali zote mbili zinatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili kusogeza karibu huduma kwa wananchi na hivyo waweze kufurahia matunda ya Muungano,” amesisitiza Mhe. Khamis.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TEA, mkurugenzi Mkuu Dkt. Erasmus Kipesha amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano (mwaka 2019/2020 – 2024/2025), Mamlaka imetekeleza miradi mbalimbali yenye thamani ya takribani sh. bilioni 2.8.

Amefafanuwa kuwa kati ya hizo, sh. Bilioni 2.1 zimetumika kuboresha miundominu ya elimu wakati sh. milioni 574.3 zimefadhili Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi (SDF) kwa vijana 600 kutoka kaya maskini.

Pamoja na maeneo hayo pia Kamati ilipata wasaa wa kutembelea na kukagua kiwanja ambacho kutajengwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itayojengwa Zanzibar.

Ziara hiyo pamoja na viongozi mbalimbali iliwashirikisha Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi na wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Taasisi hizo.

Hii ni ziara ya kwanza kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kufanya ziara katika Taasisi za Muungano zilizopo katika upande wa Zanzibar.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi