





==================================================================================================================
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa ameuomba uongozi wa Mkoa wa Geita kufanya ukaguzi wa mabwawa yenye tope sumu katika migodi, hasa kuelekea msimu wa mvua.
Kwagilwa ametoa agizo hilo baada ya kutembelea eneo la Msasa, lenye mgodi wa wachimbaji wadogo katika Wilaya ya Bukombe, akitaka Mkoa kwa kushirikiana na Tume ya Madini, NEMC na Mamlaka za Mabonde ya Maji kutembelea migodi ya kati na mikubwa na kujiridhisha kuhusu usalama wa mabwawa hayo.
“Ni muhimu tukajiridhisha kuwa endapo mvua itanyesha ikasababisha maji kujaa na kuleta mafuriko tujiridhishe kwamba tumechukua tahadhali kabla jambo hilo halijatokea ni muhimu sana.” Amesema Mhe. Kwagilwa.
Akisisitiza maandalizi dhidi ya mvua za El Niño, Mhe. Kwagilwa ameuagiza uongozi wa mgodi wa Msasa kuhakikisha unajenga mitaro inayowezesha maji kutiririka vizuri, na walizko kwenye maduara waongeze pampu za kusukuma maji ili kuzuia maji kutuama katika mashimo hayo.
Aidha, amewasihi wananchi kuendelea kufanya usafi na kutoa ushirikiano kwa uongozi ili miundombinu hiyo ijengwe kwa wakati, hatua ambayo amesema itasaidia kunusuru mgodi huo dhidi ya changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa za El Niño na kuwalinda wananchi pamoja na mazingira.