
Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa akizungumza wakati wa kikao na uongozi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira nchini, kikoa kilichofanyika leo, Aprili 13, 2026, jijini Dodoma katika Ofisi za Makamu wa Rais zilizopo mji wa serikali Mtumba.


Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Sarah Kibonde (katikati), akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wakuu wa TBC na Ofisi ya Makamu wa Rais kilichofanyika leo Aprili 13, 2026, Dodoma, ambapo walijadiliana masuala ya mawasiliano ya serikali na uelimishaji wa umma kuhusu mazingira.




Mkurugenzi wa Habari na Matukio wa TBC, Bi. Eshe Muhidini, alipohudhuria katika kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wakuu wa TBC na Ofisi ya Makamu wa Rais kilichofanyika leo Aprili 13, 2026, Dodoma, kikilenga kuimarisha ushirikiano katika utoaji wa taarifa na uhamasishaji wa masuala ya mazingira kwa umma.
========================================================================================================
Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Ofisi hiyo, Bi. Sarah Kibonde wamekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu utunzaji wa mazingira nchini.
Kikao hicho kimefanyika leo, Aprili 13, 2026, jijini Dodoma katika Ofisi za Makamu wa Rais zilizopo mji wa serikali Mtumba.
Mazungumzo hayo yamelenga kuboresha mikakati ya mawasiliano ya umma ili kuhakikisha ujumbe wa uhifadhi wa mazingira unawafikia wananchi kwa ufanisi zaidi kupitia vyombo vya habari, hususan redio na televisheni na mitandao ya kijamii.
Katika kikao hicho, pande zote mbili zilikubaliana kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu athari za uharibifu wa mazingira na umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kulinda rasilimali asilia.
Aidha, walisisitiza haja ya kuandaa vipindi maalum vya elimu kwa umma vitakavyojikita katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, uhifadhi wa misitu, usimamizi wa taka, pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali za maji.
Mkurugenzi wa Mazingira Bi. Mutasa alieleza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais ina jukumu la kusimamia na kuratibu masuala ya mazingira nchini, hivyo ushirikiano na taasisi za habari kama TBC ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa sera na mikakati ya mazingira.
Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano huo, wananchi watahamasika zaidi kushiriki katika shughuli za utunzaji wa mazingira, ikiwa ni pamoja na upandaji miti na kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Bi Sarah Kibonde alisisitiza umuhimu wa kutumia lugha rahisi na inayoeleweka kwa wananchi wote ili kuhakikisha ujumbe wa mazingira unawafikia watu wa rika na makundi mbalimbali.
Alibainisha kuwa kampeni za mawasiliano zitapangwa kwa kuzingatia maeneo yenye changamoto kubwa za kimazingira ili kuleta matokeo chanya.
Aidha, katika kikao hicho, ilielezwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya upandaji miti yatakayofanyika Juni 5, mwaka huu.
Kutokana na umuhimu wa tukio hilo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Bi Sarah Kibonde aliomba Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuanza mapema kuligusia na kulipa uzito katika vipindi vyake ili kuufahamisha umma kuhusu maandalizi na umuhimu wa kushiriki katika zoezi hilo la kitaifa.
Alisisitiza kuwa uhamasishaji wa mapema utasaidia kuongeza mwitikio wa wananchi katika upandaji miti, hatua itakayochangia juhudi za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira nchini.
Naye Mkurugenzi wa Habari na Matukio wa TBC, Bi. Eshe Muhidin, aliahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa kutoa kipaumbele kwa vipindi vinavyohusu mazingira pamoja na kuongeza muda wa kurusha matangazo ya elimu kwa umma.