
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira Mhe. Reuben Kwagilwa akizungumza wakati wa mafunzo kwa Wabunge kuhusu Biashara ya Kaboni, Mafanikio, Changamoto na Hatua za Utatuzi wake yaliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) jijini Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira Mhe. Reuben Kwagilwa (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Maduhu Kazi wakifuatilia mafunzo kwa Wabunge kuhusu Biashara ya Kaboni, Mafanikio, Changamoto na Hatua za Utatuzi wake yaliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) jijini Dodoma.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria pamoja na Kamati ya Maji na Mazingira wakiwa katika mafunzo kwa Wabunge kuhusu Biashara ya Kaboni, Mafanikio, Changamoto na Hatua za Utatuzi wake yaliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) jijini Dodoma.

Viongozi mbalimbali wakishiriki katika mafunzo kwa Wabunge kuhusu Biashara ya Kaboni, Mafanikio, Changamoto na Hatua za Utatuzi wake yaliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) jijini Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira Mhe. Reuben Kwagilwa (katikati) na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Maduhu Kazi (wa tatu kulia) akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) Dkt. Albina Chuwa (wa pili kulia), Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo Khamis Hamza Khamis na watendaji wakiwa katika picha ya pamoja katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma mara baada ya mafunzo kwa Wabunge kuhusu Biashara ya Kaboni, Mafanikio, Changamoto na Hatua za Utatuzi wake yaliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
=============================================================================
Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) imetoa mafunzo kwa Wabunge kuhusu Biashara ya Kaboni, Mafanikio, Changamoto na Hatua za Utatuzi wake.
Mafunzo hayo yaliyofanyika leo Agosti 13, 2026 jijini Dodoma yametolewa kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria pamoja na Kamati ya Maji Mazingira.
Akifungua mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro alisema ili miradi ya kaboni iendelee kufanyika kwa ufanisi ni muhimu mifumo ikasomana.
Dkt. Ndumbaro ambaye pia ni Mbunge wa Songea Mjini alisema Ofisi ya Makamu ni muhimu kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii yenye dhamana ya misitu pamoja na Wizara ya Nishati ambayo ina jukumu la kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali za nishati.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa wabunge kwakuwa wao ndio wawakilishi wa wananchi katika maeneo yao hivyo itakuwa rahisi kufikisha ujumbe kwa urahisi.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Prof. Pius Yanda alisema inapaswa kuyageuza mabadiliko ya tabianchi kuwa fursa kwa kushiriki katika biashara ya kaboni.
Prof. Yanda ambaye pia ni Mbunge wa Buhigwe alisema ni muhimu kutumia fursa ya uwepo wa biashara ya kaboni kwa kuhakikisha uendelevu wa bioanuwai nchini.
Awali akitoa maelezo mafupi, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira Mhe. Reuben Kwagilwa alisema mafunzo hayo ni mojawapo ya mikakati ya kuhakikisha elimu ya hifadhi ya mazingira inaifikia jamii.
Alisema Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuyafikia makundi mbalimbali katika kuhakikisha wanakuwa na uelewa kuhusu suala la biashara ya kaboni na hivyo kutumia fursa kujipatia kipato.
Mhe. Kwagila aliongeza kuwa Tanzania ina fursa kubwa kupitia rasilimali za misitu, bahari, maziwa, mito na ardhi zenye uwezo mkubwa wa kufyonza na kuhifadhi gesijoto.
Aidha, katika kuchagiza na kuhamasisha jamii katika matumizi ya nishati safi ya kupikia tayari majiko safi 900,000 yametolewa kwa kaya zaidi ya 600,000 katika mikoa yote 26.
Pamoja na mambo mbalimbali, mafunzo hayo yalikwenda sanjari na elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo inaelezwa kuwa Tanzania inatumia Biashara ya Kaboni kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mafunzo hayo yalihudhuriwa pia Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Maduhu Kazi, watendaji kutoka Ofisi ya Makamu Rais, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni na watendaji kutoka Benki ya CRDB.