Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu Rasmi ya Ofisi ya Makamu wa Rais

Tanzania yatoa wito kukabili kupanda kwa kina cha bahari
Sep 25, 2026
Tanzania yatoa wito kukabili kupanda kwa kina cha bahari
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, akihutubia Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kupanda kwa kina cha Bahari, uliyofanyika kando ya Mkutano wa 18 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA81), New York – Marekani.
Na Robert Hokororo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, akihutubia Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kupanda kwa kina cha Bahari, uliyofanyika kando ya Mkutano wa 18 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA81), New York – Marekani.

===========================================================================================

Tanzania imetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuongeza kasi ya upatikanaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi, teknolojia na mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema ili kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari zinazoongezeka za kupanda kwa kina cha bahari.

 

Akihutubia Mkutano wa Ngazi ya Juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kupanda kwa kina cha Bahari mjini New York, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amesema tatizo hilo si tishio la siku zijazo tena, bali tayari linaathiri maisha ya watu, uchumi na mifumo ya ikolojia duniani.

 

Kwa Tanzania, athari hizo ni kubwa kutokana na ukanda wake wa pwani ya Bahari ya Hindi, Zanzibar na visiwa vingine ambavyo vinategemewa na mamilioni ya watu kupitia uvuvi, utalii na biashara. Mmomonyoko wa fukwe, kuingia kwa maji ya chumvi katika vyanzo vya maji baridi na mafuriko vinatajwa kuwa miongoni mwa vitisho kwa wananchi, miundombinu na mafanikio ya maendeleo ya nchi.

 

Makamu wa Rais ameeleza kuwa, Tanzania tayari inachukua hatua kwa kuimarisha ulinzi wa pwani, kurejesha mikoko na mifumo ya ikolojia, kuimarisha usalama wa maji na kuendeleza mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inayoongozwa na jamii.

 

Hata hivyo, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa juhudi za nchi moja moja hazitoshi, akitaka fedha za tabianchi kuwa za kutosha, za uhakika na zinazopatikana kwa urahisi zaidi kwa nchi zinazoendelea na jamii za pwani zilizo katika mazingira hatarishi.

 

Mkutano huo wa Septemba 24, 2026, umezikutanisha nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, Viongozi, Wataalamu na Wadau wengine kuweka  msimamo wa pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa dhidi ya tishio la kupanda kwa kina cha bahari. Mkutano huo unafanyika ikiwa ni mwendelezo wa Mkutano wa Ngazi ya Juu wa mwaka 2024 uliolifanya suala hilo kuwa ajenda muhimu ya kimataifa.

 

Miongoni mwa maeneo ya msingi yanayopewa uzito ni ulinzi wa maisha na shughuli za kiuchumi katika maeneo ya pwani, mifumo ya tahadhari za mapema, takwimu za tabianchi, miundombinu himilivu, teknolojia, suluhisho zinazotegemea mazingira asilia pamoja na kuongeza uwezo wa nchi zilizo hatarini kukabiliana na athari zisizoepukika.

 

Mkutano huo unatarajiwa kufikia Azimio la pamoja lenye mwelekeo wa utekelezaji, likilenga kuimarisha hatua za kimataifa, ustahimilivu na uwezo wa kukabiliana na kupanda kwa kina cha bahari.

 

Tanzania imeunga mkono kupitishwa kwa Azimio hilo kwa makubaliano ya pamoja, huku ikisisitiza umuhimu wa dunia kuhamisha mjadala kutoka katika ahadi kwenda kwenye utekelezaji wenye matokeo.

 

Kwa Tanzania, utekelezaji wa dhamira hizo unaweza kufungua fursa zaidi za ushirikiano wa kimataifa katika rasilimali za tabianchi, teknolojia, mifumo ya tahadhari za mapema na ujenzi wa miundombinu himilivu, hatua zenye umuhimu mkubwa katika kulinda jamii za pwani hususani Zanzibar, sekta ya utalii, uvuvi na shughuli nyingine za uchumi wa buluu.

 

Akihitimisha ujumbe wake, Makamu wa Rais ametoa mwito wenye msisitizo kwa jumuiya ya kimataifa: “Bahari inatuunganisha. Hivyo basi, kupanda kwa kina cha maji yake kunapaswa pia kutuunganisha katika kuchukua hatua za pamoja.”

 

Makamu wa Rais yuko New York nchini Marekani, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi

slot gacor