

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Bw. Stphen Ndaki akizumgumza Juni 6, 2026 akiwa mkoani wakati kwenye kikao na wadau wa biashara ya kaboni kwenye kikao ambacho kimefanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.



===================================================================================================================
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema kuwa maendeleo na ukuaji wa biashara ya kaboni nchini yanapaswa kwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akisisitiza kuwa sekta hiyo ni miongoni mwa nyenzo muhimu zitakazochochea ukuaji wa uchumi, uhifadhi wa mazingira na ustawi wa wananchi katika kipindi cha miongo ijayo.
Dkt. Muyungi alitoa kauli hiyo leo Juni 6, 2026 mkoani Kagera wakati alipokutana na wadau wa biashara ya kaboni katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera. Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa serikali, wataalamu wa mazingira, wadau wa sekta binafsi pamoja na wawakilishi wa taasisi zinazojihusisha na biashara ya kaboni.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Muyungi alisema Serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha kuwa biashara ya kaboni inasimamiwa kwa ufanisi ili iweze kutoa manufaa ya kiuchumi kwa wananchi huku ikiendelea kuimarisha juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Alieleza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unaotarajiwa kuanza Julai 1, 2026 unatoa nafasi kubwa kwa sekta mbalimbali, ikiwemo biashara ya kaboni, kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya taifa.
Alisema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili, hususan misitu, ambayo inaweza kutumika kuzalisha mikopo ya kaboni (carbon credits) na hivyo kuongeza mapato kwa wananchi na taifa kwa ujumla. Aidha, alibainisha kuwa biashara ya kaboni imeendelea kuwa moja ya fursa mpya za kiuchumi duniani kutokana na kuongezeka kwa jitihada za kimataifa za kupunguza uzalishaji wa gesi joto zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.
“Serikali inaendelea kuweka mazingira bora yatakayowezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika biashara ya kaboni ili waweze kunufaika na fursa zinazotokana na sekta hii. Tunahitaji kuhakikisha kuwa ukuaji wa sekta hii unaendana na malengo ya maendeleo ya taifa na matarajio yaliyowekwa katika Dira ya 2050,” alisema Dkt. Muyungi.
Katibu Mkuu huyo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi katika kuhakikisha kuwa biashara ya kaboni inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa jamii zinazoshiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira. Aliongeza kuwa elimu kwa umma kuhusu fursa za biashara ya kaboni ni muhimu ili wananchi waweze kuelewa thamani ya rasilimali walizonazo na namna ya kuzitumia kwa maendeleo endelevu.
Aidha, aliwataka wadau wa biashara ya kaboni kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali ili kuhakikisha kuwa shughuli zote zinazofanyika zinakuwa na uwazi, uwajibikaji na manufaa kwa pande zote zinazohusika.