Serikali imesema imepokea jumla ya dola za Marekani milioni 320 katika kipindi cha mwaka 2024/25 hadi 2025/26 ili kuboresha na kurejesha miundombinu muhimu iliyoharibika kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Pia, kwa kuzingatia hilo imesema itaendelea kuhakikisha kuwa masuala ya mabadiliko ya tabianchi ambayo Ofisi ya Makamu wa Rais inasimamia yanazingatiwa kikamilifu katika mipango na bajeti.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27 leo Juni 11, 2026.
Alisema athari za mabadiliko ya tabianchi zinaikumba Tanzania, hali inayoathiri sekta muhimu za uchumi hususan kilimo, maji, afya, uchukuzi na nishati hivyo Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana nazo.
Katika kukabiliana nazo, Balozi Omar alisema kuwa Serikali imeanzisha matumizi ya utaratibu wa dharura chini ya Benki ya Dunia kwa ajili ya kukabiliana na athari za majanga yanayotokana na changamoto hizo.
Kwa upande mwingine, alisema Serikali itaendelea kutoa motisha katika matumizi ya nishati safi ikiwemo ujenzi wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya matumizi katika shughuli mbalimbali ikiwemo kupikia, viwandani pamoja na usafiri na usafirishaji.
Balozi Omar alifafanua kuwa lengo la kutoa motisha hiyo ni kuhakikisha uwepo wa nishati salama na endelevu, kuokoa muda, kupunguza gharama pamoja na athari za kimazingira na kiafya kwa watumiaji.
Hatua hiyo itachangia katika kuhifadhi mazingira kwa wananchi na taasisi kutumia nishati safi kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa yanayotokana na ukataji wa miti.
Aidha, alisema pamoja na Mikakati mbalimbali Serikali itaendelea pia kutekeleza Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032), Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia (2024–2034).