Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu Rasmi ya Ofisi ya Makamu wa Rais

Italia kuwekeza biashara ya kaboni Tanzania
Jun 15, 2026
Italia kuwekeza biashara ya kaboni Tanzania
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi alikifanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa wa Nchi za Ulaya, Wizara ya Mazingira na Usalama wa Nishati ya Italia Bi. Ambra Migliorisi, kikao kilichofanyika Juni 14, 2026, jijini Bonn, Ujerumani wakati wa Mkutano wa 64 wa Kamati za Utekelezaji na Sayansi na Ushauri chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ukiendelea.
Na Robert Hokororo

==========================================================================================================

Ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SJMT) na Serikali ya Italia umeleta manufaa nchini ambapo taifa hilo limeonesha nia ya kufanya uwekezaji katika biashara ya kaboni na hifadhi ya mazingira kwa ujumla.

Hayo yamebainika wakati Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kimataifa wa Nchi za Ulaya, Wizara ya Mazingira na Usalama wa Nishati ya Italia Bi. Ambra Migliorisi aliyeambatana na Naibu Mtendaji Mkuu wa Shirika la kimataifa la Sustainable Energy for All (SEforALL) lenye makao makuu jijini Vienna, Austria Bw. Stefano Marguccio. 

Kikao hicho kimefanyika Juni 14, 2026, jijini Bonn, Ujerumani wakati wa Mkutano wa 64 wa Kamati za Utekelezaji na Sayansi na Ushauri chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ukiendelea

Aidha, mazungumzo hayo yalilenga katika kukuza ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na nchi ya Italia ambayo imevutiwa na mazingira yaliyopo ya uwekezaji nchini. 

Wizara ya Mazingira na Usalama wa Nishati ya nchini humo imeonesha nia ya kuwekeza nchini kwenye biashara ya kaboni hasa katika utekelezaji wa Ibara ya 6.2 ya Mkataba wa Paris kuhusu kuhusu ushirikiano wa utekelezaji wa biashara ya kaboni. 

Kati ya nchi 14 zilizoainishwa barani Afrika, Tanzania imechaguliwa na kupewa kipaumbele katika uwekezaji huo kutokana na uwepo wa Sera, Kanuni, Miongozo na mifumo mizuri ya uendeshaji wa Biashara ya Kaboni pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo.

Sanjari na hilo, Serikali ya Italia kupitia Wizara ya Mazingira na Usalama wa Nishati ambayo imedhamiria kuwekeza kwa kuanza na miradi ya majaribio kwa kushirikiana na Mtaalamu Elekezi kutoka Shirika la SEforALL aliyepewa kandarasi ya kufanya upembuzi yakinifu utakaowezesha kufanyika kwa uwekezaji huo.

Dkt. Muyungi, aliishukuru Serikali ya Italia kupitia wizara hiyo kwa kuendeleza na kukuza ushirikiano na uhusiano wa miaka mingi na kuikaribisha kuwekeza nchini kwakuwa masuala ya uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya mazingira yamepewa kipaumbele katika nguzo ya tatu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alisema biashara ya kaboni ni mojawapo ya maeneo ya kipaumbele katika kuongeza mapato ya nchi kupitia shabaha iliyowekwa kwenye Dira 2050 ya ukusanyaji wa Dola za Kimarekani bilioni mbili katika eneo la biashara hiyo pamoja na Uchumi wa Buluu, hivyo ili kufikia lengo hilo ni muhimu kufanyika jitihada mahsusi katika kuongeza na kukuza ushirikiano na uhusiano na nchi mbalimbali ili kupata wawekezaji wengi.

Pia, Dkt. Muyungi aliueleza Ujumbe huo kuwa ni muhimu kuzingatia sekta za kimkakati za kipaumbele ambazo zimebainishwa na Tanzania kuhusiana na biashara hiyo hususan eneo la Nishati, Taka (Waste), Usafirishaji, Viwanda, Kilimo, Uchumi wa Buluu ambazo zote zinapewa kipaumbele na SJMT na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kuanza mara moja mchakato wa kuandaa Mkataba wa Makubaliano (MoU) na Mkataba wa Ushirikiano.

Halikadhalika, kupitia mazungumzo hayo, alihimiza Serikali ya Italia kuanza mara moja mchakato na mawasiliano rasmi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuharakisha mchakato wa uwekezaji huo. 

Mkutano huo unafanyika kuanzia Juni 8 hadi 18, 2026 ukiwakutanisha wataalamu wa mabadiliko ya tabianchi kutoka katika nchi zote wanachama wa mkataba huo kujadili na kukubaliana misimamo ya nchi zinazoendelea katika maeneo mbalimbali ya majadiliano kuendana na makundi ya Afrika na nchi zinazoendelea.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawakilishwa na wataalamu kutoka Wizara za Kisekta, Taasisi za Umma, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, Vijana na Watoto.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi

slot gacor