
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akimfariji Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, mara baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Mazishi ya Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo iliyofanyika, katika Kanisa la Hija ya Bikira Maria - Pugu Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 28 Februari 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, mara baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Mazishi ya Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo iliyofanyika, katika Kanisa la Hija ya Bikira Maria - Pugu Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 28 Februari 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Viongozi wa Kanisa Katoliki, wakishuhudia mwili wa aliyekua Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ukiteremshwa kaburini, wakati wa mazishi yaliyofanyika katika Kituo cha Hija – Pugu Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 28 Februari 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiweka udongo katika kaburi la aliyekua Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, wakati wa mazishi yaliyofanyika katika Kituo cha Hija – Pugu Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 28 Februari 2026.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiweka shada la maua katika kaburi la aliyekua Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, wakati wa mazishi yaliyofanyika katika Kituo cha Hija – Pugu Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 28 Februari 2026.
======================================================================
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mazishi ya Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, yaliyofanyika katika Kanisa la Hija ya Bikira Maria - Pugu Jijini Dar es Salaam.
Akitoa salamu za rambirambi mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Mazishi, Makamu wa Rais amesema Serikali inathamini uzalendo na mchango mkubwa aliyoutoa Kardinali Pengo katika maendeleo ya nchi, kiroho na kimwili. Amesema Kardinali Pengo, alijitoa kwa moyo sio kwa wakatoliki tu bali kwa watanzania wote wenye imani tofauti, kila mahali alipoweza kufanya utume wake.
Makamu wa Rais, amesema Kardinali Pengo alikuwa mtu mwadilifu ambaye alisisitiza watu kuishi Maisha ya kiadilifu kwa kufuata na kushika amri za Mungu pamoja na kufuata sheria mbalimbali za nchi. Pia alifundisha na kuyaishi maadili katika siku zote za maisha yake. Amesema ni vema kila Mtanzania kujikumbusha wajibu wake kwa nchi na kuishi kwa vitendo mambo yote mazuri yanayotokana na maisha ya Kardinali Pengo.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba, Kardinali Pengo atakumbukwa kwa kupenda sana maendeleo na ustawi wa jamii. Alijitoa katika kuinua hali za watu na kuwaletea maendeleo watanzania,alifanya jitihada kubwa katika upatikanaji wa huduma mbalimbali za jamii, hususani elimu, afya , maji na huduma kwa watu wenye mahitaji maalum.
Amesema inapaswa kuenzi mchango wake wa maendeleo katika nchi kwa kuwa waadilifu na watiifu wa sheria.
Makamu wa Rais, ametoa wito kwa Watanzania kutambua wajibu wa msingi wa kuitumikia nchi kwa uadilifu na uaminifu. Amewaomba viongozi wa dini kuendelea kuwaombea Viongozi wa nchi ili waweze kutenda vema kazi zao.
Makamu wa Rais ametoa salamu za pole kwa Kanisa Katoliki Tanzania na Ulimwenguni kote, wakristo wakatoliki, ndugu jamaa na marafiki kufuatia msiba huo mkubwa. Amemuombea marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo apate pumziko la amani Mbinguni.
Marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amezikwa katika Kituo cha Hija ya Bikira Maria – Pugu Jijini Dar es Salaam.