==============================================================================================================
Serikali imesema utekelezaji wa miradi ya biashara ya kaboni hasa kaboni ya buluu utakapokamilika na mauzo kufanyika, itanufaisha jamii inayozunguka maeneo mengi ya Ukanda wa Pwani.
Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma leo Juni 16, 2026 na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maryam Azan Mwinyi aliyetaka kufahamu ni maeneo gani ya Ukanda wa Pwani yamenufaika na Blue Carbon.
Mhe. Kwagilwa alisema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC) imeendelea kusajili miradi mbalimbali ya biashara ya kaboni nchini hususan kaboni ya buluu inayofyonzwa na kuhifadhiwa na mazingira ya baharini na pwani kama vile misitu ya mikoko na nyasi za bahari hivyo husaidia kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza kipato cha jamii za pwani.
Alitaja miradi iliyosajiliwa katika maeneo ya ukanda wa pwani kuwa ni pamoja na Mradi wa Mimbiki uliopo Chalinze, Mradi wa Mikoko Carbon Sink uliopo Mkinga, Mkuranga, Tanga Mjini na Pangani.
Miradi mingine ni Mradi wa Carbon for Farmers uliopo mikoa ya Pwani, Tanga, Lindi na Mtwara, Mradi wa Organic West Composite Tanzania uliopo Mkuranga na Mradi wa Buyuni Redd+ Farm Carbonuliopo Mkoa wa Pwani, ambayo yote ipo katika hatua za awali za utekelezaji.
Akiendelea kujibu swali hilo Mhe. Kwagilwa alibainisha kuwa biashara ya bluu kaboni ni eneo la kipaumbele kwa nchi ambalo limewekewa msisitizo katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Serikali kupitia Sera ya Uchumi wa Bluu ya mwaka 2023 pamoja na Mkakati wake wa utekelezaji, imeweka kipaumbele cha kuanzisha miradi ya bluu kaboni na kuvutia wawekezaji kuwekeza katika biashara hiyo, kwa lengo la kunufaisha jamii za pwani na kuongeza pato la Taifa,” alisema.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na eneo kubwa la ukanda wa pwani ya bahari lenye fursa kubwa ya kaboni ya buluu hivyo, Serikali imeanza kutoa elimu ili wananchi watambue fursa hizo.
Alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Maryam aliyeuliza kuhusu mikakati ya Serikali katika kutoa elimu ya buluu kaboni ili wananchi wanufaike hususan wanawake.
Akijibu swali hilo, Mhe. Kwagilwa alisema eneo la bahari linakadiriwa kufikia kilomita za mraba zaidi ya 60,000 na eneo la ukanda wa uchumi wa bahari ni kilomita za mraba 223,000 wakati eneo la mikoko lina hekta 147,000 ambalo linafaa kwa jamii kulitumia kukuza uchumi.
“Kutokana na hali hiyo sisi kama Serikali imetufanya kuanza kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo vya habari na pia tumetoa elimu kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kule Zanzibar, tunataka elimu ifikie hadi shuleni ili watambue fursa hizo za kaboni ya buluu,” alisema.
Mhe. Kwagilwa alimalizia kwa kusema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kushirikiana taasisi za elimu kikiwemo Chuo Kikuu cha Zanzibar na wadau wanaotarajia kuwekeza kwenye biashara ya kaboni ya buluu kwa kujisajili NCMC.