
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Kamani ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais alipotembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maonesho ya kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma Agosti 04, 2026.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Kamani ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais alipotembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maonesho ya kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela jijini Dodoma Agosti 04, 2026.
===========================================================================================================
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Kamani ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendelea kuhamasisha ushiriki wa wadau katika masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
Naibu Ng’wasi amesema hayo Jumanne Agosti 4, 2026 Jijini Dodoma wakati alipotembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maonesho ya kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Malecela.
Amesema mazingira ni sekta mtambuka inayogusa shughuli zote za maendeleo ya kijamii na kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi na hivyo ni muhimu kwa wadau wote kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali.
“Sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi tunaguswa moja kwa moja na masuala ya mazingira, tunaipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendelea kuhakikisha wadau wote wanashiriki katika juhudi za Serikali za kuhamasisha uhifadhi na utunzaji wa mazingira” amesema Mhe. Ng’wasi.
Aidha Naibu Waziri Ng’’wasi amesema ushiriki wa wadau ni muhimu katika kipindi hiki ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa malengo nguzo ya tatu ya Dira 2050 inayohusiana na masuala ya uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.
Awali akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Ng’wasi, Afisa Mazingira Mwandamizi Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Lungo amesema Ofisi hiyo imeendelea kuimarisha ushirikiano na wadau katika kuhakikisha elimu ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira inaifikia jamii kupitia njia mbalimbali.
“kwa kutumia nyenzo mbalimbali ikiwemo nyaraka, vitabu, vipeperushi na makala mjongeo kupitia maonesho haya tumeendelea kuwaelimisha wananchi kuhusiana na majukumu yanatekelezwa na Ofisi” amesema Lungo.
Akiwa katika banda la Ofisi ya Makamu wa Rais, Naibu Waziri Ng’wasi alipata elimu kuhusu masuala ya Muungano pamoja na kufahamishwa mafanikio yanayoendelea kupatikana katika masuala ya Muungano, Mazingira na Uchumi wa Buluu.