Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu Rasmi ya Ofisi ya Makamu wa Rais

Serikali kuanzisha Mpango wa Mageuzi ya Kijani
Mar 15, 2026
Serikali kuanzisha Mpango wa Mageuzi ya Kijani
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza wakati wa ziara ya kikazo mkoani Geita Machi 14 ,2026.
Na Robert Hokororo

===========================================================================================================

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amepongeza Mkoa wa Geita kwa jitihada zake katika uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Masauni ametoa pongezi hizo Machi 24,2026 wakati wa ziara yake mkoani humo, akifuatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Muyungi , pamoja na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, wataalamu wa mazingira na viongozi kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shegella amesema mkoa huo umechukua hatua mbalimbali kulinda mazingira, ikiwemo kushirikiana na wataalamu wa mazingira kudhibiti baadhi ya shughuli za wachimbaji wadogo wa madini zinazoweza kuharibu mazingira.

Amesema baadhi ya wachimbaji hao hutumia miti kama matimba wakati wa kushuka kwenye migodi, jambo linalochangia ukataji wa miti. Kutokana na hilo, serikali ya mkoa imeendelea kutoa elimu na kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za mazingira pamoja na kuhakikisha wachimbaji wadogo wanafukia mashimo mara baada ya kumaliza shughuli za uchimbaji.

Katika juhudi za kuhifadhi mazingira, Shegella amesema mwaka 2025 mkoa huo ulifanikiwa kupanda miti milioni 3.5 kama sehemu ya mkakati wa kupambana na uharibifu wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Mkoa wetu umeingia katika utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa yanayolenga kudhibiti matumizi ya zebaki katika shughuli za uchimbaji madini ifikapo mwaka 2030,” amesema

Akizungumzia umuhimu wa Muungano wa Tanzania, Mkuu huyo wa Mkoa amesema umechangia kuimarisha mshikamano wa kitaifa, akibainisha kuwa katika shughuli za uchimbaji madini mkoani Geita kuna wachimbaji wengi wadogo kutoka Zanzibar ambao wamekuja kuchangamkia fursa za kiuchumi.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Muyungi, ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Geita kwa kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Kanda ya NEMC, ambalo ni la kwanza kujengwa nje ya makao makuu ya taasisi hiyo.

Amesema jengo hilo litakuwa la kisasa na la mfano, likiwa na ofisi pamoja na maktaba ambayo itatumika kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi wa kanda husika

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi