
Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa, akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya Kitaifa ya maandalizi ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani (WED 2026) kilichofanyika tarehe 4 Mei 2026. Maadhimisho hayo hufanyika tarehe 5 Juni kila mwaka.





Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa, ametoa wito kwa Wizara, Taasisi za serikali, Sekta binafsi pamoja na wadau wote wa mazingira nchini kushirikiana kwa karibu katika maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani (WED), yatakayofanyika tarehe 5 Juni 2026.
Akizungumza leo Mei 4, 2026 jijini Dodoma, katika Ofisi za Makamu wa Rais zilizopo Mtumba, Bi. Mutasa alisisitiza umuhimu wa mshikamano na uratibu mzuri ili kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanyika kwa mafanikio na kuleta tija kwa Taifa.
Bi. Mutasa alieleza kuwa Siku ya Mazingira Duniani ni jukwaa muhimu la kimataifa linalotumika kuhamasisha uelewa wa umma kuhusu uhifadhi wa mazingira na kuchochea hatua za kukabiliana na changamoto za kimazingira kama vile mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira, na upotevu wa bioanuai.
Hivyo, alisisitiza kuwa maandalizi yake yanapaswa kuzingatia ushirikishwaji mpana wa wadau wote ili kufikisha ujumbe kwa jamii kwa ufanisi zaidi.
Aidha, aliwataka wajumbe wa kamati hiyo kuhakikisha wanabuni mikakati madhubuti ya kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira, ikiwa ni pamoja na kampeni za upandaji miti, usafi wa mazingira, na matumizi sahihi ya rasilimali asilia.
Pamoja na hayo alisisitiza umuhimu wa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe kwa wananchi wengi zaidi, hasa vijana.
Katika kikao hicho, ilielezwa kuwa maandalizi yanaendelea vizuri, huku baadhi ya shughuli zilizopangwa zikijumuisha maonesho ya teknolojia rafiki kwa mazingira, mijadala ya kitaalamu, pamoja na shughuli za kijamii zitakazofanyika sambamba na kilele cha maadhimisho hayo Juni 5, 2026.
Kwa upande wao, wajumbe wa kamati hiyo walimhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa wataendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanyika kwa ufanisi mkubwa na kuendana na malengo ya kitaifa na kimataifa katika kulinda na kuhifadhi mazingira.
Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 Juni, ikiwa ni juhudi za kimataifa zinazoongozwa na Umoja wa Mataifa kuhamasisha uhifadhi wa mazingira. Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine duniani, huadhimisha siku hiyo kwa kufanya shughuli mbalimbali zinazolenga kuongeza uelewa na kuchochea hatua za kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu.
Maadhimisho ya mwaka 2026 yatafanyika Mkoani Dodoma na yanatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha juhudi za taifa za kukabiliana na changamoto za kimazingira, huku yakihimiza ushiriki wa kila mwananchi katika kulinda rasilimali za nchi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.