




Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yaliyofanyika tarehe 01 Mei 2026 katika Uwanja wa Jamhuri.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amewataka watumishi wote wa umma kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uwajibikaji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kwa wakati.
Alisisitiza kuwa mchango wa watumishi wa umma ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo ya taifa.
Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kauli mbiu isemayo, “Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2025,” ikihimiza umuhimu wa ajira zenye staha katika kuchochea maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.
“Ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kuhakikisha anatimiza majukumu yake kwa bidii na kwa kuzingatia maadili ya kazi, ili kuendana na matarajio ya wananchi na malengo ya Serikali,” alisema Rosemary Senyamule.
Aidha, aliwataka watumishi kuzingatia nidhamu ya kazi, kutumia rasilimali za umma kwa uangalifu na kushirikiana kwa karibu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku, akibainisha kuwa ushirikiano ni msingi muhimu wa mafanikio ya mipango ya maendeleo.
Kwa upande wa maadhimisho ya kitaifa, yalifanyika Mkoani Njombe yakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alisisitiza umuhimu wa kulinda haki za wafanyakazi, kuboresha mazingira ya kazi na kuimarisha uchumi jumuishi.
Maadhimisho ya Mei Mosi hufanyika kila mwaka ikiwa ni fursa ya kutambua mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhisho endelevu.