Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu Rasmi ya Ofisi ya Makamu wa Rais

Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais washiriki Mei Mosi kitaifa Njombe
May 01, 2026
Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais washiriki Mei Mosi kitaifa Njombe
Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais wakishiriki katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), 2026 kitaifa mkoani Njombe leo Mei Mosi, 2026.
Na Robert Hokororo

Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais wameungana na wafanyakazi wengine nchini kutoka Wizara, Idara, Taasisi, Mashirika ya Umma na Binafsi katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), 2026.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliongoza mamia na maelfu ya wafanyakazi hao katika maadhimisho hayo ambayo kitaifa yamefanyika Mkoani Njombe.


Wakiwa katika maadhimisho hayo Watumishi wa Ofisi wa Makamu wa Rais walishiriki tukio la maandamano ya wafanyakazi nchini ambapo walibeba mabango yaliyoakisi kauli mbiu ya maadhimisho na majukumu yanayotekelezwa na Ofisi hiyo. 


Mabango hayo yaliakisi majukumu yanayotekelezwa na ofisi ambayo ni masuala ya Muungano, Mazingira na Uchumi wa Buluu. 


Katika bango lenye maudhui ya Muungano, watumishi hao walibeba ujumbe unaoeleza umuhimu wa Muungano katika kuimarisha Umoja na Mshikamano huku maudhui ya masuala ya mazingira yakieleza umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia. 


Itakumbukwa kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuhimiza jamii kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ili kulinda mazingira. 


Ujumbe mwingine kuhusu mazingira ulieleza kampeni ya upandaji miti ya '27 ya kijani, Mti wa Mama' iliyoasisiwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo inaenda sambamba na tarehe yake ya kuzaliwa ikilenga kuhimiza jamii umuhimu wa kupanda miti. 
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi