
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi leo Julai 23, 2026 jijini Dodoma akifanya mazungumzo na viongozi wa Tanzania Carbon Developers Association (TACADEVA).




Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati za kuimarisha usimamizi wa biashara ya kaboni nchini ili kuiwezesha sekta hiyo kuwa miongoni mwa vyanzo muhimu vya mapato ya taifa, sambamba na kutekeleza malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema Serikali imejipanga kujenga mfumo imara wa usimamizi wa biashara ya kaboni ili Tanzania inufaike kikamilifu na fursa zinazotokana na soko la kimataifa la kaboni, huku ikihakikisha sekta hiyo inachangia ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu.
Dkt. Muyungi alitoa kauli hiyo leo Julai 23, 2026 jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Tanzania Carbon Developers Association (TACADEVA).
Alisema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukiimarisha Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (National Carbon Monitoring Centre – NCMC), ikiwemo kuongeza wataalamu wenye utaalamu wa masuala ya kaboni, kuboresha mifumo ya kidijitali ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya kaboni, pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuongeza uwezo wa taasisi hiyo.
Kwa mujibu wa Dkt. Muyungi, hatua hizo zinalenga kujenga mfumo madhubuti wa usimamizi wa biashara ya kaboni utakaoongeza uwazi, ufanisi na kuiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na fursa zinazotokana na soko la kaboni duniani.
"Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha biashara ya kaboni inakuwa sekta yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na kuongeza mapato ya taifa, kama ilivyoelekezwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," alisema Dkt. Muyungi.
Alibainisha kuwa, kuthibitisha dhamira hiyo, Serikali imetenga Shilingi bilioni 5 katika Mwaka wa Fedha 2026/27 kwa ajili ya shughuli za Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), hatua inayolenga kuongeza uwezo wa kituo hicho katika kusimamia na kufuatilia biashara ya kaboni kwa ufanisi zaidi.
Aidha, alisema Serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuongeza uwezo wa sekta hiyo, akieleza kuwa Serikali ya Norway imekubali kutoa ufadhili wa Dola za Marekani milioni tano kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa NCMC na kuboresha mfumo wa usimamizi wa biashara ya kaboni nchini.
Katika mazungumzo hayo, viongozi wa Tanzania Carbon Developers Association (TACADEVA) waliwasilisha changamoto mbalimbali za kiutendaji zinazoikabili sekta ya biashara ya kaboni nchini, wakieleza kuwa baadhi ya changamoto hizo zimekuwa zikisababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya kaboni na hivyo kupunguza kasi ya maendeleo ya sekta hiyo.
Akijibu hoja hizo, Dkt. Muyungi aliwahakikishia wadau hao kuwa Serikali inazitambua changamoto hizo na tayari imeweka mikakati madhubuti ya kuzitatua ili kuondoa vikwazo vinavyoathiri maendeleo ya biashara ya kaboni nchini.
Alisema hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali, ikiwemo kuimarisha uwezo wa NCMC, kuongeza wataalamu, kuboresha mifumo ya kidijitali na kuimarisha uratibu wa taasisi zinazohusika na biashara ya kaboni, zitaleta ufanisi zaidi katika utoaji wa huduma na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kaboni nchini.
Dkt. Muyungi aliwahimiza wadau hao kuendelea kushirikiana na Serikali katika kubaini na kutatua changamoto zinazoendelea kujitokeza, akisisitiza kuwa lengo la Serikali ni kujenga mazingira rafiki yatakayowezesha biashara ya kaboni kukua, kuvutia uwekezaji na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tanzania Carbon Developers Association (TACADEVA), Bi. Rehema Mbalamwezi, aliipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua katika kuimarisha usimamizi wa soko la biashara ya kaboni nchini.