
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt Richard Muyungi akipanda Mtu muda mfupi baada ya kuwasili katika Kijiji cha Matebete kilichopo, tarafa ya Ilongo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya ambapo alifika kijijini hapo leo Mei 25, 2026 kwa ajili ya Kuzindua Kiwanda cha Kusindika Maziwa kilichotengenezwa kwa ufadhili wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi wa Bayoanuai Tanzania (SLR) unaotekelezwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt Richard Muyungi (kulia) akipokea heshima ya kuvalishwa vazi la asili ya Kimasai (mgolori) na Mwenyekiti wa Kijiji cha Matebete, Bw. Lokordu Eliakimu (kushoto). Dkt. Muyungi alifika kijijini hapo leo Mei 25, 2026 kwa ajili ya Kuzindua Kiwanda cha Kusindika Maziwa kilichotengenezwa chini ya Ufadhi wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi wa Bayoanuai Tanzania (SLR) uliopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt Richard Muyungi akiswaga ng'ombe kuingia kwenye josho jipya ambalo limejengwa na Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi wa Bayoanuai Tanzania (SLR). Tukio hilo limefanyika leo Mei 25, 2026 katika Kijiji cha Matebete kilichopo tarafa ya Ilongo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya ambapo Dkt. Muyungi alifika hapo kwa ajili ya uzinduzi wa Kiwanda cha Kusindika Maziwa.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Richard Muyungi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais waliombatana naye katika uzinduzi wa Kiwanda cha Kusindika Maziwa uliofanyika leo Mei 25, 2026, katika Kijiji cha Matebete, Tarafa ya Ilongo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt Richard Muyungi akionesha zawadi ya 'culture' aliyopewa na wananchi wa Kijiji cha Matebete kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya ikiwa ni ishara ya kumkaribisha mara baada ya kufika leo Mei 25, 2026 Kuzindua Kiwanda cha Kusindika Maziwa kilichotengenezwa kwa ufadhili wa Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi wa Bayoanuai Tanzania (SLR) uliopo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.



==========================================================================================================
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, ametoa wito kwa wananchi na wanufaika wa miradi ya maendeleo nchini kuhakikisha wanaitunza na kuiendeleza miradi inayotekelezwa na Serikali pamoja na wadau wa maendeleo, ili iweze kuendelea kutoa manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo sambamba na kuchochea safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050.
Dkt. Muyungi ametoa kauli hiyo leo Mei 25, 2026 wakati wa ziara yake katika vijiji vya Matebete na Nyangulu vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya, alipokuwa akizindua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofadhiliwa kupitia Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR), unaotekelezwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akizungumza mbele ya wananchi, viongozi wa serikali za vijiji, wataalamu wa sekta mbalimbali pamoja na wanufaika wa miradi hiyo, Dkt. Muyungi alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza nguvu kubwa katika utekelezaji wa miradi yenye tija kwa wananchi, hususan katika maeneo ya uzalishaji mali, uhifadhi wa mazingira na kuinua uchumi wa wananchi wa vijijini.
Alisema mafanikio ya miradi hiyo hayatategemea tu uwekezaji wa Serikali na washirika wa maendeleo, bali pia ushiriki wa wananchi katika kuitunza miundombinu iliyojengwa pamoja na kuhakikisha inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, ni muhimu kwa wanufaika kuhakikisha miradi hii inalindwa, inatunzwa na kuendelezwa ili iweze kudumu na kuendelea kuwa msaada katika kufikia azma ya taifa ya kuwa na uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050,” alisema Dkt. Muyungi.
Akiwa katika Kijiji cha Matebete kilichopo Tarafa ya Ilongo, Kata ya Itamboleo, Dkt. Muyungi alizindua Mradi wa Kiwanda cha Kusindika Maziwa unaokadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 200.
Mradi huo unatajwa kuwa miongoni mwa miradi muhimu inayolenga kuimarisha sekta ya mifugo na kuongeza thamani ya mazao ya mifugo kwa wananchi wa eneo hilo.
Fedha zilizotolewa kupitia mradi huo zimetumika kujenga miundombinu mbalimbali ya mifugo ikiwemo josho, kibanio, birika pamoja na kisima kirefu cha maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
Aidha, fedha hizo pia zimetumika kujenga kiwanda cha kusindika maziwa kitakachosaidia kuongeza thamani ya maziwa yanayozalishwa na wafugaji wa eneo hilo.