Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Hassan Chande akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wadau wanaomiliki kumbi za Starehe, Wadau wa Muziki, Wamiliki wa Bendi na Wamiliki wa baa katika warsha iliyoandaliwa na NEMC kuhusu sualala kelele na mitetemo kwa Wadau hao.
Sehemu ya Wadau waliohudhuria warsha hiyo inayohusu  mitetemo na sauti kwa Wadau mbalimbali wakiwemo Wamiliki wa kumbi za starehe, wamiliki wa Baa, Wamiliki wa Bendi na Wadau wa Muziki jijinI Dar es Salaama iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

==========================================================================

Ukuaji wa maendeleo ya nchi kiuchumi unachangia changamoto mbalimbali katika mazingira kama, mabadiliko ya tabianchi, kelele na mitetemo na changamoto nyingine.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Hamad Hassan Chande, leo Septemba 30, 2021 mkoani Dar es Salaam wakati akifungua Warsha kwa Wamiliki wa Kumbi za Starehe, Bendi za Muziki, Baa na Wadau wa Muziki na kuandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Alisema kwasababu ya changamoto hizo ameona ni vizuri kukutana na wadau hao ili wapatiwe elimu kuhusu kelele na mitetemo ili kulinda na kuokoa Mazingira na afya ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

“Tumeona kuna umuhimu mkubwa wa kukutana pamoja ili kutoa elimu kuhusu kelele na mitetemo ili kulinda Mazingira na afya ya vizazi vyetu vya sasa na vijavyo,” alisema Mhe. Chande.

Aliongeza kuwa kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la kelele na mitetemo katika maeneo yanayozunguka jamii zinazotokana na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

“Tafiti mbalimbali duniani na hapa nchini zimefanyika zinaonesha kwa sasa kelele na mitetemo ni changamoto kubwa inayokuja kuathiri afya za wananchi wetu. Mfano, Shirika la Afya Duniani (WHO) limebainisha kelele ni kisababishi cha madhara katika maisha ya binadamu. Aidha, ‘European Environmental Agency’ katika ripoti yao ya mwaka 2018 imeonesha kuwa kelele inachangia vifo vya mapema vya watoto, watoto takribani 12,000 kila mwaka hufariki katika Bara la Ulaya,” alisema.

Aliongeza hapa nchini kuna tafiti zinaendelea na NEMC wameanza jitihada hizo katika Kanda mbalimbali, Mfano Kanda ya Kaskazini wamefanya tafiti ndogo kuhusu kelele na mitetemo mkoani Arusha na umeonesha kuwa kelele na mitetemo ni changamoto katika jamii. Wananchi wengi wameonesha kuathirika moja kwa moja. Katika utafiti huu, maeneo yaliyoongoza kwa kusababisha kelele chafuzi ni maeneo ya starehe kwa asilimia 33 na Viwanda asilimia 24.

Alizitaja baadhi ya athari ni kuathirika kwa akili na kusababisha wasiwasi, msongo, hofu, kichefuchefu, maumivu ya kichwa, ubishi, mabadiliko ya hisia kwenye tendo la ndoa “sexual impotence”, Kuharibika kwa utendaji wa kazi na matatizo ya kupoteza kumbukumbu na  Usumbufu wa usingizi ambapo hali hii husababisha kuwa na shinikizo la damu, mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida hutokea (haraka au polepole).

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Mhandisi Dkt. Samuel Gwamaka alisema hivi karibuni Baraza limepokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu matukio yanayohusiana na kelele na mitetemo. Hivyo ndiyo maana Baraza limeandaa warsha hiyo kwa Wadau hao.

”Katika kulitafutia ufumbuzi jambo hili kwa kushirikiana na Wizara mbalimbali,  kwa pamoja kama Serikali tumekubaliana kelele na mitetemo ni janga linalokuja kwa kasi katika jamii yetu. Pamoja na kuwepo Sheria mbalimbali za kisekta, pia tumeandaa Mwongozo wa udhibiti wa uchafuzi wa Mazingira utokanao na Kelele na Mitetemo ambao unaonesha muundo wa wadau wa utekelezaji wa udhibiti kelele na mitetemo,” alimalizia Dkt. Gwamaka.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *