=============================================================================================

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Saidi Jafo ameteua wajumbe saba wa Kamati itakayofanya kazi ya kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu uboreshaji wa elimu katika Muungano.

Akizungumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar Jafo alisema uteuzi huo umefanyika ikiwa ni hatua ya kushughulikia maoni yaliyotolewa na wadau mbalimbali kuhusu tofauti ya ufaulu wa wanafunzi wa Shule za Sekondari za Tanzania Bara na Zanzibar kwa matokeo mbalimbali ya Kidato cha Nne na Sita.

Pamoja na maoni hayo alisema pia wabunge mbalimbali wamekuwa wakiwasilisha hoja hiyo wakati wa mjadala wa bajeti ya mwaka 2021/22 wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Jafo ameipa kamati hiyo siku 35 kukamilisha kazi ya kushughulikia maoni hayo na kuwasilisha taarifa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ili kwa kushirikiana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi waweze kukaa na mawaziri wanaohusika na masuala ya elimu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwashauri namna bora ya kuboresha elimu pande zote mbili za Muungano.

“Kamati niliyoiteuwa itafanya kazi kwa kipindi kisichozidi siku 35 nami kwa haraka nikutane na wenzangu wanaohusika na sekta ya elimu kwa lengo la kuboresha hata yake maandalizi ya vijana wa kidato cha nne na sita ili tuweze kuwapa ushauri kutoka timu ya wataalamu wetu nini inasema katika kuboresha hili,” alisema.

Aidha Waziri jafo aliwataja wajumbe walioteuliwa kuwa ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Taaluma, Utafiti na Huduma

kwa Umma), Prof. Alexander Boniface Makulilo ambaye atakuwa Mwenyekiti     na Makamu wake ni Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Zanzibar Mhe. Najma Murtaza Giga ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Wajumbe watakaounda kamati ni mdau wa elimu sekta binafsi Abdulmarik Mollel, Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za Serikali, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Khalid Bakari Hamrani, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), Dkt. Charles Msonde, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Gerald Mweli na Mkufunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Zanzibar (IPA), Said Hamad Shehe.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *