Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akizungumza na Viongozi mbalimbali walioshiriki katika kutafuta ufumbuzi hoja 11 za Muungano  wakati wa Utiaji saini wa hati  za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi. Hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii,Maruhubi, Zanzibar Agosti 24,2021.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa hati  za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi. Hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii,Maruhubi, Zanzibar Agosti 24,2021.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa hati  za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi. Hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii,Maruhubi, Zanzibar Agosti 24,2021.
Matukio mbalimbali wakati wa hafla ya utiaji saini wa hati  za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi. Hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii,Maruhubi, Zanzibar Agosti 24,2021.

============================================================================

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amesema utaratibu wa kutafuta ufumbuzi wa hoja za Muungano kupitia mazungumzo una nia ya kuuenzi na kuulinda Muungano thabiti uliopo.

Dkt. Mpango alisema hayo wakati wa hafla ya utiaji saini wa hati za makubaliano ya kuondoa hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Utalii, Maruhubi, Zanzibar Agosti 24, 2021.

Pia alitoa rai kwa taasisi zote husika kuhakikisha changamoto zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi na zile zitakazojitokeza, ni muhimu kuzitambua mapema, kuzijadili kwa uwazi na umakini ili kuzitafutia ufumbuzi kwa manufaa ya pande zote mbili za Muungano.

Aliziagiza Wizara za Fedha na Mipango za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ0 kuchukua jitihada za makusudi kuzitafutia ufumbuzi hoja zinazohusu ushirikiano katika masuala ya fedha ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi.

Aidha, Makamu wa Rais alisisitiza sekta zote kuendeleza vikao vya kisekta kwa pande zote mbili za Muungano ili kupunguza hoja zinazoletwa kwenye kamati ya Pamoja.

Kwa Upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alimuhakikishia Makamu wa Rais kwamba ofisi yake itaendelea kuratibu vizuri na kwa weledi mkubwa katika kutatua kero mbalimbali zinazojitokeza kwa wananchi katika masuala ya Muungano.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Abdullah alisema kusainiwa kwa hati hizo kutaondosha migongano kwa vizazi vya sasa na baadae pamoja na kuwaleta maendeleo wananchi na wawekezaji wa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hapo Awali Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango aliongoza kikao cha kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kushughulikia masuala ya muungano kilichofanyika katika ukumbi wa Idriss Abdul Wakili Zanzibar, kikao kilichopitisha kwa pamoja kuondolewa hoja 11 za muungano zilizopatiwa ufumbuzi.

———

Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Abdullah, Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Hussein Katanga, Katibu wa Mkuu Kiongozi Zanzibar Mhandisi Zena Said, Mawaziri, Makatibu wakuu kutoka pande zote za muungano pamoja na viongozi wengine.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *