Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo, akipewa ufafanuzi na Mkurugenzi wa kiwanda cha Chilambo General Tradingcompany Bwa. Gidion Chilambo, namna wanavyofanya shughuli zao kiwandani hapo, kilichopo Kisarawa Mkoa wa Pwani.
Sehemu ya bidhaa chakavu za kielektroniki zitakazo chakatwa na kugeuzwa kuwa malighafi ya bidhaa nyingine.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo, akitoa maelekezo baada ya kufika kiwanda cha Prayosha Industries Limited kilichopo Kisarawe Mkoa wa Pwani.

=========================================================================

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo ameupongeza uongozi wa kiwanda cha Chilambo General Trade Company kwa kushiriki katika usafi wa mazingira kwa kukusanya taka za kielektroniki ili zisiweze kusambaa hovyo mitaani.

Jafo ametoa pongezi hizo leo Agosti 10, 2021 alipofanya ziara katika kiwanda hicho kinachochakata taka za kielektroniki kuwa malighafi ya kuzalisha bidhaa, kilichopo wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani kujionea namna wanavyofanya shughuli zao bila kuathiri Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004.

“Ofisi ya Mazingira ipo tayari kuwapa msaada na muongozo kuhakikisha viwanda vyao vinasimama pamoja na kuwapa vibali ambavyo itawasaidia kufanya shughuli zao bila bugudha wala uchafuzi wowote wa Mazingira,” alisema.

Waziri Jafo aliongeza kuwa wawekezaji wote wanaotaka kufanya shughuli ya namna hii wataendelea kupewa miongozo ya kimazingira juu ya namna gani watafanya shughuli zao bila ya kuathiri mazingira. 

Alisema Chilambo General Trade Company inatarajia kuanzisha kiwanda kipya cha kurejeleza taka za kielektroniki lakini wanatakiwa kuhakikisha wanakamilisha mchakato wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kwa lengo la kuujua vizuri mradi na athari za kimazingira kabla ya kuanzisha mradi, hii itasaidia kuepusha uingizwaji wa taka ambazo hazitafaa kwa matumizi ya kiwanda.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Bw. Gideon Chilambo alisema wanazingatia Sheria ya Mazingira na wanacho cheti cha mazingira ila kwa kiwanda wanachotarajia kufungua watafanya Tathmini ya kimazingira kama alivyoagiza Waziri Jafo ili kuepusha uchafuzi wa mazingira.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo alitembelea kiwanda cha Prayosha Industries Limited kinachozalisha malighafi ya sabuni kilichopo Kisarawe kujionea hali ya kimazingira na amekipongeza kiwanda hicho kwa kuzingatia sheria ya mazingira.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *