Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais   Bi. Mary Maganga akizungumza wakati wa Hafla ya kusaini Mkataba wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais Awamu ya pili, Mtumba jijini Dodoma leo Oktoba 13, 2021.Jengo hilo litagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 18.8 na  linajengwa na SUMA JKT kwa kipindi cha miezi 24.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga (wa nne kushoto mbele) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali baada ya Hafla ya kusaini Mkataba wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais Mtumba jijini Dodoma leo Oktoba 13, 2021

Ofisi ya Makamu wa Rais imesaini Mkataba wa Shilingi Bilioni 18.8 na Kampuni ya ujenzi ya SUMA JKT wa kuanza awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

Hafla ya kusaini Mkataba wa ujenzi huo imefanyika katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mtumba jijini Dodoma Oktoba 13, 2021 na kukabidhi rasmi eneo la ujenzi kwa Mkandarasi baada ya kushinda zabuni, na kushuhudiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambaye ndio Msimamizi Elekezi wa ujenzi wa jengo hilo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga ameipongeza SUMA JKT kwa kushinda kandarasi hiyo na kutaka ujenzi uwe wa haraka kwa kuzingatia ubora, viwango na kasi.

“Ninaamini kuwa SUMA JKT mna uzoefu mkubwa, na ujenzi huu utaenda kwa kasi, na kuzingatia viwango vya ubora wa hali ya juu, na ikiwezekana mkamilishe kazi hii kabla ya muda uliopangwa,” amesema Bi. Mary Maganga.

Aidha, Katibu Mkuu alisema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu kwa kuwa Serikali ilipohamia Dodoma jengo lililojengwa katika eneo la Mtumba halitoshelezi mahitaji ya watumishi wote hivyo kulazimika kutumia jengo lingine mjini kwa ajili ya watumishi wa idara zingine.

“Wenzetu wa Idara ya Mazingira wapo wengi na wana majukumu mengi kila tunapowahitaji kuja kwa ajili vikao inabidi waje huku Mtumba kwa hiyo jengo hili likikamilika ndani ya muda tuna imani ufanisi utaongezeka na tunaweza kufanya kazi kwa pamoja na muda tunaotumia barabarani utapungua au kuondoka kabisa” alisema.

Aidha, Bi. Mary Maganga amesema, msimamizi wa ujenzi huo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) atafanya kazi kwa karibu na Kamati ya Ujenzi ya Ofisi ya Makamu wa Rais inayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Bw. Mohammed Khamis Abdullah na kusisitiza kutenga Ofisi kwa ajili ya Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *