===========================================================================

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa muda wa miezi sita kwa uongozi wa Bandari ya Mtwara kufanyia marekebisho ya dosari za kimazingira zilizobainika.

Ametoa maelekezo hayo Desemba 20, 2011 alipofanya ziara ya kikazi katika bandari hiyo kwa ajili ya kufuatilia uzingatiaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004.

Dkt. Jafo ameelekeza uongozi wa bandari hiyo kuandaa eneo maalumu lililokidhi vigezo litakalotumika kuhifadhi makaa ya mawe yanayosafirishwa baada ya kubaini yanahifadhiwa katika eneo lingine lisilokidhi vigezo.

Hata hivyo kwa kuanzia aliagiza kufanya ukaguzi wa kimazingira katika eneo wanalotumia hivi sasa kuhifadhia makaa hayo mawe kwa kufuata utaratibu wa sheria.

Alisema bandari hiyo inafanya vizuri katika sekta ya uchukuzi na ina umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi hivyo inapaswa kuwa mfano bora wa kufuata masharti yote ya mazingira yanayotakiwa.

“Tulitoa cheti kwa ajili ya kuhifadhi makaa ya mawe na makaa haya ni heavy metal, cheti kile hakitoki kama kadi ya harusi na ndio maana nilitaka nikione. Bandari mlielekzwa mtenge eneo maalumu la kuyahifadhi lakini mmeamua kwenda sehemu nyingine na watu wangu wa NEMC (Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira) waliwapiga faini, tunataka bandari yetu ifanye vizuri kwa kufuata kanuni zilizowekwa na Serikali,” alisisitiza.

“Binafsi nafarijika kuona korosho zinasafirishwa kupitia bandari hii na hii inaonesha namna miundombinu ya barabara inavyotunzwa na mnatoa ajira kwa vijana wetu hapa na pia simenti inapitia hapa kwa hiyo uchumi unakua,” alisema.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Kusini, Mhandisi Boniface Guni alisema bandari hiyo ilipata Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA) mwaka 2019 na kupewa masharti mbalimbali.

Miongoni mwa masharti hayo ni kuweka miundombinu ya kudhibiti uchafuzi unaotokana na maka ya mawe ikiwemo vumbi na maji ya mvua ambayo yanaweza kuingia baharini pindi yakitiririka kwenye makaa hayo.

Meneja Guni alibainisha hata hivyo eneo cheti kilichoelekeza bandari haikutumia na badala yake ilianza kutumia eneo lingine ambalo kwa mujibu wa cheti lina mapungufu.

Naye Meneja wa Bandari ya Mtwara, Bw. Norbert Kalembo alisema wameyapokea maelekezo ya Waziri Jafo yakiwemo kufanya ukaguzi wa kimazingira na kuahidi kuyafanyia kazi.

Alisema Bandari ya Mtwara imekuwa ikijihusisha na shughuli za kupokea na kusafirisha makaa ya mawe, saruji na korosho.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *