============================================================================

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameagiza Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kwa kushirikiana na mamlaka ya jiji la Dodoma pamoja na ofisi ya mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais kuhakikisha wanalinda Bustani za miti zilizoanzishwa Dodoma pamoja na kuhamasisha wananchi kupanda miti ili kukabiliana na ukame katika jiji hilo.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati alipotembelea na kukagua Bustani za miti zilozopo eneo la Medeli jijini Dodoma zinazomilikiwa na TFS pamoja na Bustani inayomilikiwa na jiji la Dodoma.

Ameagiza mamlaka ya jiji la Dodoma kusimamia taasisi za serikali, binafsi pamoja na wafanyabiashara waliopo kandokando ya barabara kuhakikisha wanapanda miti na kuisimamia ili kupendezesha jiji la Dodoma pamoja na kukabiliana na ukame. Amewata wataalamu kutoka idara ya mazingira kuacha kukaa ofisi badala yake kwenda kwa wananchi kuwasaidia katika upandaji miti.

Amewataka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kutoa elimu ya miti kwa wananchi mara kwa mara ili kuepusha wananchi kupanda miti inayoweza kuharibu vyanzo vya maji pamoja na kuharibu majengo. Makamu wa Rais ameagiza uongozi wa jiji la Dodoma kutumia sheria zilizopo katika kukabiliana na waharibifu wa mazingira ikiwemo uchomaji moto maeneo yaliopandwa miti.

Aidha ameagiza katika upangaji wa miji kuhakikisha kunazingatia maeneo ya kilimo pamoja na bustani za miti ili kutopoteza maeneo yote katika ujenzi wa majengo na baadae kusababisha ukame katika jiji la Dodoma.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ametembelea na kukagua bustani ya miche inayozalishwa na wakala wa misitu Tanzania TFS eneo la Mailimbili jijini Dodoma. Makamu wa Rais Dkt. Mpango ameagiza TFS kuzalisha miche mingi zaidi pamoja na kuanzisha vitalu vipya vya miche ili kuongeza kasi ya upandaji miti kwa wananchi wanaohitaji miche hiyo. Amesema mpango wa serikali ni kuifanya Dodoma kuwa ya kijani na kuanzia mwaka 2022 kampeni hiyo inatarajia kubadili muonekano wa mji huo.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *