============================================================================

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameelekeza Manispaa ya Mtwara Mikindani kuhakikisha inalinda eneo la dampo kisasa lililojengwa lisivamiwe na wanachi.

Dkt. Jafo ametoa maelekezo hayo Desemba 20, 2021 alipofanya ziara ya kikazi katika dampo hilo mkoani Mtwara lenye eneo la ukubwa wa ekari 23 kwa ajili ya kukagua namna wanavyosimamia taka ngumu.

Alisema baadhi ya wananchi wana tabia kuvamia maeneo yaliyo karibu na madampo kisha kujenga nyumba na kufanya makazina huishia kutupia lawama kwa Serikali ya eneo husika kuhusu harufu mbaya inayotokana na taka hizo.

Alisema Serikali ilitafuta fedha ili kuhakikisha madampo yanajengwa katika maeneo kadhaa hapa nchini katika kuhakikisha kunawepo na usimamizi mzuri wa taka ngumu.

Waziri Jafo alitumia nafasi hiyo kuipongeza manispaa hiyo kwa kuwa na usimamizi mzuri wa taka zinazotupwa katika dampo hilo hali inasaidia kutunza mazingira ya mji.

 “Nimekuja kuangalia dampo hili namna mnavyozishughulikia taka ngumu na kweli nimekuta taka zote zinatupwa hapa tofauti na baadhi ya madampo huko nilipopita ambako taka hazitupwi kabisa kabisa dampo zinaachwa zinazagaa ovyo,” alisema.

Kwa upande wake Ofisa Mazingira wa manispaa hiyo, Bw. Masumbuko Mtasigwa alisema yapo malori manne ambayo yanatumika kusafirisha taka kutoka katika vizimba 25 vilivyopo katika kata 18.

Hata hivyo alibainisha changamoto ya gharama za uendeshaji kwa maana ya usafirishaji kupitia malori hayo pamoja na uwepo wa taka nyingi za plastiki kutupwa.

Naye Meneja wa Kanda ya Kusini wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mhandishi Boniface Guni alisema changamoto ya matumizi ya vifuko vidogo vya plastiki visivyo na viwango bado ipo.

Alisema hiyo ni kutokana na kuingia kwa magendo lakini Baraza hilo linaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mifuko mbadala rafiki wa mazingira na kuendesha operesheni ya kukamata mifuko iliyopigwa marufuku.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *