===========================================================================

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameitaka Halmashauri ya Iringa kukamilisha mradi wa machinjio ikiwemo mfumo wa majitaka uanze kufanya kazi.

Ametoa maelekezo hayo Januari 25, 2022 wakati alipofanya ziara katika manispaa hiyo kwa ajili ya kukagua ujenzi wa machinjio hayo uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 na kuhamasisha upandaji miti kwa wanafunzi.

Dkt. Jafo alionesha wasiwasi kwa kutokamilika mradi huo akisema kuwa hali hiyo inaweza kusababisha mazingira kuendelea kuchafuliwa kutokana na uchinjaji holela na umwagaji majitaka ovyo katika makazi ya watu.

“Leo nimekuja hapa interest yangu kubwa ni kukagua mazingira kule mtachinja wanyama na mwisho wa siku majitaka yataingia katika mfumo huu majitaka sasa shaka yangu ni spidi ya kukamilisha mradio huu, bila huu mradi watu watachinja ovyo bila kuzingatia mazingira,” alitahadharisha.

Hata hivyo, Waziri Jafo aliridhishwa na muundo wa mfumo wa majitaka unaooendelea kujengwa sambamba na machinjio hiyo na kusema kuwa umekidhi vigezo vya kimazingira ikiwemo kutibu majitaka hayo.

Kwa upande wake Mchumi wa Manispaa, Bw. Herbert Bilia alisema mradi huo uliibuliwa mwaka 2008 kwa ajili ya kuanza kutekelezwa lakini ulikamwa mwaka 2015 kutokana na changamoto za kifedha.

Bw. Bilia alibainisha kuwa mradi huo wenye thamani ya sh. bilioni 1. unaotekelezwa kupitia fedha za mapato ya ndani, Serikali Kuu pamoja na wadau wa maendeleo, ulifufuliwa tena mwaka 2019 5/16 na kutakiwa kukamilika Desemba 31, 2021.

Mchumi huyo aliongeza kuwa matarajio ya Manispaa na Mkoa huo ni kuona mkandarasi huyo anakamilisha mradi huo kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma.

Aidha, katika ziara hiyo Waziri Jafo alizindua Kampeni ya upandaji miti kwa wanafunzi wa shule na vyuo maarufu kama ‘Soma na Mti katika Mkoa wa Iringa kupitia wanafunzi wa Shule ya Sekondari na wasichana Iringa.

Aliongoza zoezi la upandaji wa miti kwa wanafunzi, walimu na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Moyo ambapo alitoa hamasa kwa wanafunzi hao kupanda mti mmoja mmoja kwa kila mwanafunzi ili kuhifadhi mazingira na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *