Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt Selemani Jafo akisisitiza jambo wakati wa ziara yake ya kutembelea ghala ya kuhifadhia kemikali aina ya salfa linalomilikiwa na Kampuni ya African Inland Logistics Ltd katika Kata ya Sandali wilayani Temeke mkoani Datr es Salaam. Alitembelea ghala hilo baada ya kupata taarifa juu ya umwagaji wa kemikali hiyo katika maeneo ya karibu na ghala hilo.
Mmoja wazee anayejulikana kwa jina la Abdalah Magulu akitoa maoni yake kuhusiana na uchafuzi wa umwagaji wa kemikali aina ya salfa katika Kata ya Sandali wilayani Temeke  mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo wakati alipofanya ziara kutembelea eneo hilo.

====================================================================

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa siku saba kwa Kampuni ya African Inland Logistics Ltd. kusimamisha kazi zote wanazofanya kuhusiana na usafirishaji na utunzaji wa kemikali ya salfa, katika ghala lake ili kufanya marekebisho katika usafirishaji na uhifadhi wa kemikali hiyo pasipo kuhatarisha afya za wananchi wa eneo hilo.

Ameyasema hayo leo wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam katika Kata ya Sandali alipofanya ya kutembelea na kufanya ukaguzi katika ghala hilo.

“Natoa maelekezo kwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kusimamisha shughuli zote za ghala hili mpaka watakapofanya marekebisho katika usafirishaji na uhifadhi wa kemikali hii ya salfa katika ghala hili ambalo liko katika makazi ya watu, tunapenda uwekezaji katika Nchi yetu lakini uwekezaji ni lazima kutunza afya za Wananchi. Wahakikishe wanaposafirisha kemikali hii hamna hata punje moja inayomwagika,” alisema.

Aidha Waziri Jafo ameelekeza kampuni hiyo pia kufanya ukaguzi wa mazingira (environmental audit) mara moja kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira inavyotaka. “Ninyi mnafanya kazi wakati hamna cheti cha aina yoyote, naagiza kufanya kaguzi ya mazingira, tunapenda uwekezaji uende mbele lakini siyo kudhuru wananchi kama hivi mnavyofanya,” alielekeza.

Akiongea katika ziara hiyo Meneja NEMC Kanda ya Kusini Mashariki Bwana Hamad Taimuru amewataka wenye ghala hilo kutumia mifuko maalumu ya kufungashia kemikali (jumbo bags) ili kuepusha umwagaji hovyo barabarani wa kemikali hiyo ya salfa wakati wa usafirishaji wake kutoka bandarini kwenda kwenye ghala hilo.

Naye Diwani wa Kata ya Sandali Mhe. Christopher Kabalika amemshukuru Waziri Jafo kwa kutembelea eneo hilo na kujionea hali halisi iliyopo eneo hilo ambapo umwagikaji huo wa kemikali ya salfa unaleta madhara kwa wananchi wa eneo hilo.

Diwani huyo aliahidi kuwa wananchi wako tayari kutoa ushirikiano kwa uwekezaji lakini kwa madhara ya namna hii hawatakuwa tayari kuvumilia.

Kwa upande mwingine wananchi wa eneo hilo wametoa kero zao mbele ya waziri huyo kwa kulalamika kuhusiana na madhara wanayopata baada ya kemikali hiyo kumwagika katika barabara ambayo ni makazi ya watu.

Mzee Said Elihuruma alisema kwua wanapitia hali mbaya kwani watoto wanaumwa vifua na kukohoa hata watu wazima pia kuwashwa ngozi na kuvimba hivyo wanamuomba Waziri awasaidie katika suala hilo.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *