Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia Ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhifadhi wa Bahari na Rasilimali zake unaofanyika  Lisbon nchini Ureno leo tarehe 27 Juni 2022.Lengo la Mkutano huo ni kuhamasisha juhudi za Mataifa katika kufanikisha utekelezaji wa Lengo la 14 la Maendeleo Endelevu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akishiriki Ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhifadhi wa Bahari na Rasilimali zake unaofanyika  Lisbon nchini Ureno leo tarehe 27 Juni 2022.Lengo la Mkutano huo ni kuhamasisha juhudi za Mataifa katika kufanikisha utekelezaji wa Lengo la 14 la Maendeleo Endelevu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali duniani wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhifadhi wa Bahari na Rasilimali zake unaofanyika Lisbon nchini Ureno leo tarehe 27 Juni 2022.

====================================================================

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania imejitolea kikamilifu katika kuhifadhi na kutumia bahari na rasilimali zake kwa njia endelevu ili kufanikisha utekelezaji wa lengo namba 14 la maendeleo endelevu.

Makamu wa Rais amesema hay oleo tarehe 27 Juni, 2022 wakati akihutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhifadhi wa bahari na rasilimali zake unaofanyika Jijini Lisbon nchini Ureno.

Amesema Tanzania imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutenga sera, mikakati na mipango ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kudhibiti kabisa mifuko ya plastiki inayotumika mara moja. Aidha Makamu wa Rais amesema Tanzania imetunga sheria zinazoongoza usimamizi wa rasilimali za bahari pamoja fukwe.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema serikali imeendelea kufanya miradi mbalimbali inayohusiana na kusimamia, kulinda, kuhifadhi na kurejesha mifumo ikolojia ya bahari , ikiwa ni pamoja na kutenga asilimia 6.5 ya sehemu ya bahari ya Hindi kuwa Maeneo Tengefu ya Bahari, kudhibiti uvuvi haramu kwa karibu asilimia 99 pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi wa bahari kuu.

Amesema Tanzania imejaliwa kuwa na ukanda mrefu wa pwani wa takribani kilomita 1,450 na Ukanda wa Kiuchumi wa Kipekee unaofikia kilomita za mraba 223,000. Aidha ametaja eneo la maji linalochukua kilomita za mraba 64,000, hivyo kuifanya nchi kuwa tajiri kwa bionuai pamoja na uwezo mkubwa wa uchumi wa buluu ambao unasaidia, maisha ya mamilioni ya watu ikiwa ni pamoja na usalama wa chakula na njia ya usafiri.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa mataifa kuhakikisha unafanyika uwekezaji katika Sayansi, uvumbuzi na ushirikiano wakati wa kutafuta suluhisho za changamoto zinazokabili bahari. Aidha amesema kuna umuhimu wa kuunganisha nguvu na kuwekeza katika teknolojia za kibunifu za kupiga vita na kupambana na uvuvi haramu pamoja na kuhusisha jamii husika katika kuzuia uchafuzi wa bahari.

Pia Makamu wa Rais amewakaribisha wawekezaji kushirikiana na Tanzania hasa katika uhawilishaji wa teknolojia rafiki na sahihi , kujenga uwezo na utafiti ili kubuni njia endelevu za kukabiliana na changamoto zilizopo katika sekta ya bahari.

Makamu wa Rais yupo nchini Ureno kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhifadhi wa Bahari na Rasilimali zake wenye lengo la kuhamasisha juhudi za Mataifa katika kufanikisha utekelezaji wa Lengo la 14 la Maendeleo Endelevu.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *