Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo, akizungumza wakati wa ziara kwenye kiwanda cha Iron and Steel ltd kilichopo Mikocheni mkoani Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Godwin Gondwe akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo kwenye kiwanda cha Iron and Steel ltd kilichopo Mikocheni mkoani Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa kwenye ziara ya kutembelea kiwanda cha Iron and Steel ltd kilichopo Mikocheni mkoani Dar es Salaam.

====================================================================

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa pongezi kwa mwekezaji wa kiwanda cha Iron and Steel Ltd kilichopo Mikocheni mkoani Dar es Salaam kwa kuyajali, kuyahifadhi na kuyatunza mazingira.

Ametoa pongezi hizo kutokana na kiwanda hicho kutekeleza maelekezo aliyotoa ya kufanya marekebisho kwenye maeneo mbalimbali ili kutunza na kuhifadhi mazingira kiwandani hapo.

Akizungumza katika ziara hiyo Dkt. Jafo alisema kiwanda hicho kiwe mfano wa kuigwa na wawekezaji wengine kote nchini ili kuhakikisha mazingira yetu yanatunzwa ipasavyo.

“Kwa kweli nimefarijika sana na mwekezaji huyo na tunahitaji wawekezaji ambao wakipewa maagizo wanayatekeleza kwa wakati,” alisema Waziri Jafo.

Aidha Waziri Jafo aliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha wanapita katika viwanda vyote nchini ili kujiridhisha na utekelezaji wake na Kwa wale ambao hawajatekeleza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao na pia waendelee kupokea malalamiko ya wananchi na kuyatekeleza.

Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kindondoni Mhe. Godwin Gondwe alimshukuru Waziri Jafo kwa kushirikiana na Ofisi yake katika utendaji, lakini pia kutumia muda wake kutembelea kiwanda hicho akisema ziara hiyo italeta tija kwa mazingira na Taifa kwa ujumla.

Mhe. Gondwe pia aliwataka wenye viwanda wengine kuiga mfano wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira uliofanikiwa sana katika Kiwanda cha Iron and Steel

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini NEMC Bw. Arnold Mapinduzi aliainisha mambo makuu manne ambayo Baraza lilielekezwa kuyasimama ili kiwanda hicho kiyaboreshe kuwa ni kusimamia suala zima la ukusanyaji wa taka, kutafuta mbinu ya kuzuia moshi unaosambaa kwa majirani wanaozunguka kiwanda na kujenga paa kwa ajili ya kupunguza vumbi kutapakaa kwa haraka.

Nyingine ni kuhifadhi kwa usahihi bidhaa mbalimbali kama vyuma chakavu pamoja na suala la kujenga ukuta ili kutenganisha na mtaro unaobeba maji machafu ambavyo vyote kwa pamoja vimerekebishwa.

Naye Afisa Uhusiano wa Iron and Steel Ltd Bw. Idrissa Ali alisema maagizo yote manne waliyopewa wamekamilisha na kutekeleza kwa weledi na kuishukuru Serikali kwa kushirikiana nao katika ufanikishaji na utunzaji wa mazingira kwa maendeleo endelevu.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *