====================================================================

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa siku nne kwa Kikosi kazi cha kusimamia Muongozo wa usafishaji mchanga kwa Mkoa wa Dar es Salaam kuwasilisha taarifa ya ufumbuzi wa athari zinazotokana na uchimbaji wa mchanga katika Mto Msimbazi.

Amesema hayo alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua mto huo katika Kata ya Mogo Mtaa wa Kipawa jijini Dar es Salaam baada ya kupokea malalamiko kuhusiana na athari za kimazingira zinazotokana na usafishaji wa mto huo.

Hata hivyo, wakati wa ziara hiyo baada ya kusikiliza maoni ya wananchi alipata maoni yanayokinzana ambapo wengine walidai shughuli za usafishaji mto huo zimeleta athari kwa mazingira na wengine wakidai zimeleta manufaa makubwa kwa jamii inayozunguka eneo hilo.

Akizungumza baada ya maelekezo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Ng’wilabuzu Ludigija amemuhakikishia Waziri Jafo kuwa amepokea maelekezo hayo na kuahidi kuyasimamia kwa karibu.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya Mashariki- Kaskazini wa Baraza la Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira (NEMC) Bw. Arnold Mapinduzi alisema Muongozo wa usafishaji mchanga umeelekeza suala hilo lifanyike kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa.

Meneja huyo alifafanua kuwa ili kuweza kufanya shughuli hiyo ya usafishaji wa mto ni lazima kuomba vibali kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bonde la Wami Ruvu.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *