Naibu Waziri Khamis atoa rai kwa wafugaji kuizingatia hifadhi ya mazingira

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akizungumza wakati wa Mkutano wa Wadau Sekta ya Mifugo uliofanyika jijini Dodoma Desemba 19, 2022 na kufunguliwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.

===================================================================

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ametoa rai kwa wafugaji nchini kuzingatia hifadhi ya mazingira kwa kutoharibu vyanzo vya maji.

Ametoa rai hiyo Desemba 19, 2022 wakati wakati wa Mkutano wa Wadau Sekta ya Mifugo lililofanyika jijini Dodoma na kufunguliwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.

Amesema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa kimazingira, sehemu kubwa ya uchafuzi wa mazingira inatokana na shughuli za kibinadamu zikiwemo kilimo kisicho endelevu, ufugaji usio endelevu na uchimbaji wa madini usiofuata sheria za mazingira.

Mhe.Khamis amesema pamoja na kuwa ufugaji ni sekta kubwa inayokuza uchumi na kutangaza nchi yetu wafugaji wanao wajibu wa kuhakikisha wanafuata sheria za mazingira.

“Niwaombe ndugu zangu wafugaji tuhakikishe hatuchungi wala hatunyweshi maji mifugo yetu kwenye vyanzo vya maji kwani kwa kiufanya hivyo tutasababisha uharibifu wa mazingira na kuua viumbe waishio humo,” aalisema.

Aidha, naibu waziri huyo amewasisitiza wafugaji na wananchi kwa ujumla kupanda miti na kuitunza ili kusaidia kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikumba nchi yetu.

Amesema hali ni mbaya kwasababu maeneo mengi wananchi wamekata miti ovyo hali inayosababisha ukosefu wa mvua na hivyo ukame kukithiri katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Naibu Waziri Khamis amesema kuwa mifugo inahama kutafuta malisho kwasababu ukame unaosababishwa na ukosefu wa mvua uliochangiwa na ukataji miti.

“Wakati tunapita na Kamati ya Mawaziri tumeona baadhi ya maeneo yameakauka sana kwa sababu za kibinadamu zikiwemo kilimo, ufugaji au uchomaji moto ovyo kwa ajili ya kuni na mkaa, niwashauri ndugu zangu pamoja twendeni tukapande miti na kuishughulikia (kuitunza),” alisisitiza naibu waziri huyo.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *