WAZIRI wa Nchi Ofisi ya makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo Dkt. Jafo akizungumza na waandishi wa habari pamoja na sehemu ya Menejimenti ya Ofisi hiyo wakati akitoa taarifa ya uzingatiaji na utekelezaji wa Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni leo Desemba 16, 2022 jijini Dodoma.

==================================================================

Serikali imewataka wadau wa biashara ya kaboni wahuishe miradi yao na kujisajili upya kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni kilichopo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro ili iendane na matakwa ya Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni.  

Hayo yamesema leo Desemba 16,2022 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo Dkt. Jafo,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya uzingatiaji na utekelezaji wa Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni 

Amebainisha kuwa uzingatiaji na utekelezaji wa kanuni na mwongozo huo utasaidia kuboresha usimamizi mzuri wa miradi ya biashara ya kaboni inayotekelezwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta zote. 

Hivyo, amesema utekelezaji wa biashara ya kaboni utachangia kupunguza gesijoto zinazosababisha ongezeko la joto duniani na hatimae kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kuchangia katika utunzaji endelevu ya mazingira na kuleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi. 

Waziri Jafo amesisitiza kuwa uzingatiaji na utekelezaji wa Kanuni na Mwongozo wa Usimamizi wa Biashara ya Kaboni ni jukumu la wadau wote, ikiwemo Wawekezaji wa Kimataifa na wanaotoka ndani ya nchi, Wizara za Kisekta, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathiriwa na athari za mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika na hali hii inajidhihirisha kupitia matukio ya mvua zisizotabirika, ongezeko la joto, ukame na mafuriko. 

“Athari hizi za mabadiliko ya tabianchi zimeathiri sekta za kijamii na kiuchumi na maendeleo kama vile kilimo, utalii, nishati, maji, afya, mifugo na mifumo ikolojia ya bahari na ardhi, hivyo kuathiri ongezeko la pato la taifa. Aidha, ukame wa muda mrefu na mafuriko yamechangia gharama kubwa za kiuchumi, kuathiri maendeleo na maisha ya jamii za vijijini na mijini,” alisema Dkt. Jafo.

Aidha, amesema kanuni na mwongozo huo vimejikita katika kuimarisha mchango wa nchi katika jitihada za kupunguza uzalishaji wa gesijoto na hivyo kupunguza athari za mazingira.

Ameongeza kuwa kanuni hizo zinalenga kuhakikisha kuwa jamii, wadau mbalimbali wanaohusika na biashara hiyo ikiwa pamoja na Serikali kunufaika kikamilifu kutokana na faida zilizopo katika biashara ya kaboni nchini.

Kutokana na hatua hiyo alielekeza Idara ya Mazingira, Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) katika Kanda zote kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta, Sekretariati za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau wa maendeleo kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa Kanuni na Mwongozo wa Usimamizi wa Biashara za Kaboni. 

Mkutano huo umehudhuriwa pia na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *