Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano & Mazingira) Mhe. Dkt. Seleman Jafo Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mbugani kata ya Ng’ambi Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma mara baada ya kuwasili kwa ajili ya ziara na uzinduzi wa miradi mbalimbali wilayani humo

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano & Mazingira) Mhe. Dkt. Seleman Jafo akizindua mradi wa kisima cha maji na kitalu nyumba katika kijiji cha Mbugani kata ya Ng’ambi Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano & Mazingira) Mhe. Dkt. Seleman Jafo akizindua mradi wamashine ya kukamua alizeti kijiji cha Ng’ambi Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano & Mazingira) Mhe. Dkt. Seleman Jafo akizindua mradi wa josho kijiji cha Kazania Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais ( Muungano & Mazingira) Mhe. Dkt. Seleman Jafo akikagua ujenzi wa Lambo kijiji cha Kazania Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewataka wananchi kutunza miradi inayotekelezwa na Serikali ili iweze kuwanufaisha katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ametoa wito huo wakati akizindua miradi ya visima vya maji, vitalu nyumba, josho la kuogeshea mifugo na mashine ya kukamua mafuta ya alizeti wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma leo Desemba 29, 2022, miradi inayotekelezwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR).

Akizungumza na wananchi wakati wa ziara hiyo, Dkt. Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeamua kutenga fedha kutekeleza mradi huo kwa maeneo mbalimbali yenye ukame ikiwemo Mpwapwa ili kutatua changamoto zinazotokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Ndugu zangu mradi huu una thamani kubwa tumeona wenyewe hapa kupeleka maji zaidi ya kilometa moja na kuleta umeme hapa kwenye kisima hiki ni gharama kubwa kwa hiyo tuutunze mradi huu kwa maslahi mapana ya vijiji hivi,” amesema.

Aidha, Dkt. Jafo amezitaka Kamati za Maji za vijiji vya Ng’ambi na Mbugani ambako amezindua visima vya maji kuusimamia mradi huo ili uwe endelevu na kuleta faida kwa wananchi.

“Inawezekana baadae mkaongeza na tanki lingine kutoka hili moja lililopo kulingana na maelekezo ya wataalamu hivyo mtakuwa mmewezesha kupanua zaidi huduma hii na sisi kama Ofisi ya Makamu wa Rais tumetimiza jukumu letu la kuwasaidia wananchi kupambana na athari za mabadiiko ya tabianchi,” ameongeza.

Vilevile Waziri Jafo amewapongeza viongozi wilayani Mpwapwa kwa kusimamia vyema miradi hii na kusema kuwa utasaidia kujenga uchumi wa mmoja mmoja na wilaya kwa ujumla.

Katika ziara hiyo amezindua mradi wa josho katika Kijiji cha Kazania ambao utawasaidai wananchi kusaidia kuogeshea mifugo na kuwaepusha na magonjwa yakiwemo kupe.

 Amezindua miradi ya visima vitatu vitakavyonufaisha wananchi zaidi ya 5000 kwani kupitia visima hivyo watakapata maji safi.

Sanjali na hayo, Mhe. Jafo amezindua vitalu nyumba ambavyo wananchi wanalima mbogamboga pamoja nyanya kwa vikundi. Vilevile Mhe. Waziri amezindua mradi wa mashine ya kukamua alizeti katika Kijiji cha Ng’ambi, mashine ambayo hukamua tani 6.5 kwa siku na kuwasaidia wananchi hao ambao awali walifuata huduma hiyo wilayani Kongwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Bi. Mwanahamisi Ally ameahidi kushirikiana na wananchi kuutunza mradi huo ili uwe endelevu.

Amesema atashirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha wanaongeza mtandao wa maji kupitia visima hivyo vilivyozinduliwa kupitia Mradi wa EBARR ili huduma iwafikiwe wananchi wengi zaidi.

Mkurugenzi huyo ameishukuru Serikali kwa mradi huo akisema kuwa maeneo mengi ya halmashauri hiyo yamekuwa na changamoto ya maji hivyo utawanuafaisha wanachi kulima mbogamboga kupitia vitalu nyumba na kujipatia kipato.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa Mhe. George Malima amesema tatizo la maji sasa lililokuwa linaikabili baadhi ya vijiji katika wilaya hiyo sasa limetatuliwa kupitia mradi huo.

Mwananchi wa Kijiji cha Mbugani Elena Mpanda akiishukuru Serikali amesema sasa hivi shida ya maji ni historia kwakuwa visima hivyo vitawanufaisha tofauti na zamani walikuwa wanayafuata wilaya jirani ya Kongwa na kuyanunua shilingi 1,500/- kwa dumu.

“Tunaishukuru sana Serikali kwani zamani tulikuwa tunaoga mara moja kwa wiki lakini sasa hivi maji tunayo mengi tu tunayatumia pia shughuli mbalimbali zikiwemo kupikia na hata kujengea nyumba za kisasa,” amesema.

Katika ziara hiyo pia Dkt. Jafo amekagua maendeleo ya ujenzi wa malambo ya kuvunia maji katika Kijiji cha Kazania na Kiegea na kutoa maelekezo yakamilike kwa wakati.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *