Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa nchi mbalimbali Duniani kabla ya kuelekea kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) unaofanyika katika Jiji la Dubai Expo tarehe 01 Desemba, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wakati wakishiriki moja ya Mikutano kando ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) unaofanyika Dubai katika Falme za Kiarabu Desemba 01, 2023.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) unaofanyika Dubai katika Falme za Kiarabu Desemba 01, 2023.

============================================================================

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, ulioanza Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023, Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Ujumbe wa Tanzania utashirikisha Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi, Viongozi na Watalaamu kutoka Wizara za Kisekta, Idara za Serikali, Mashirika ya Umma, Vyuo Vikuu, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, Vijana na Wanahabari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo utahudhuriwa na washiriki zaidi ya 70,000 kutoka nchi takribani 190. 

Wakuu wa Nchi na Serikali wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi watahutubia katika Mkutano huo, ambapo Mheshimiwa Rais Samia atakuwa mzungumzaji wa 11 miongoni mwa Wakuu wa Nchi na Serikali takriban 160 wanaoshiriki Mkutano huo. 

Sambamba na kuhutubia Mkutano huo, Tanzania imeandaa na itakuwa mwenyeji wa Mikutano Mikuu Mitatu ya Pembezoni (High-Level Side Events) inayohusu Nishati Safi ya Kupikia, Kilimo Endelevu, na Uchumi wa Buluu. 

Katika Mkutano unaohusu nishati safi ya kupikia, Mheshimiwa Rais ataongoza viongozi wenzake kutoka nchi mbalimbali duniani na taasisi za kimataifa kuzindua Programu ya Kuwakomboa Wanawake wa Afrika Kupitia Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (African Women Clean Cooking Support Programme – AWCCSP). 

Programu hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na changamoto za afya, mazingira, uchumi na kijamii ambazo huathiri zaidi wanawake na watoto. Kutokana na kwamba wanawake hutumia muda mrefu kutafuta kuni, programu hii itawasaidia kupata muda wa kutosha kushiriki kwenye shughuli za maendeleo. 

Hali kadhalika, Mheshimiwa Rais atashiriki katika mikutano ya uwili na viongozi wa serikali za nchi mbalimbali pamoja na mashirika ya kimataifa kwa lengo la kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na nchi hizo pamoja na mashirika husika. 

Mheshimiwa Rais pia atashuhudia uwekaji saini hati nne za makubaliano baina ya Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusu ajira; ushirikiano baina ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na Chuo cha Diplomasia cha Dkt. Anwar Gargash cha Umoja wa Falme za Kiarabu; ushirikiano katika masuala ya usalama na mapambano dhidi ya ugaidi; na ushirikiano katika sekta za elimu, sayansi na ufundi. 

Kaulimbiu ya Mkutano huo ni “UNITE. ACT. DELIVER”. Kitaifa kaulimbiu ni “Kuimarisha Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi”. Lengo la kauli mbiu ni kutoa msisitizo katika matumizi ya teknolojia na mbinu bora zinazozingatia changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ili kuongeza tija katika uzalishaji, mnyororo wa thamani wa mazao na masoko. Vile vile, kauli mbiu inalenga kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika kukuza uchumi wa buluu na kuchochea maendeleo endelevu. 

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *