Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi (UNOPS) Bw. Jorge Moreira da Silva mara baada ya Mkutano wa Uwili uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) unaoendelea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu leo Desemba 4, 2023. 

===========================================================================

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameishukuru Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi (UNOPS) kuisaidia Tanzania katika miradi ya mabadiliko ya tabianchi.

Ametoa shukrani hizo wakati wa Mkutano wa Uwili uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) unaoendelea Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu leo Desemba 4, 2023. 

Katika mazungumzo hayo na Ujumbe wa UNOPS ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Bw. Jorge Moreira da Silva, Dkt. Jafo ametoa wito kwa taasisi hiyo kuendelea kusaidia miradi hiyo hususan eneo la ujenzi wa kuta katika kingo za bahari na mito.

Hali kadhalika, amechagiza uwezekano wa kupata fedha za miradi ya ujenzi wa mabwawa ya kunyweshea mifugo katika maeneo ya ufugaji ili kuepusha migogoro baina ya wakulima na wafugaji.

Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo Waziri Dkt. Jafo ameweka bayana maeneo ya vipaumbele zikiwemo nyanda kame zinazoathiriwa na ukosefu wa maji kwa wakulima na wafugaji.

Kwa upande mwingine viongozi hao wamekubaliana kuendelea kushirikiana katika kushughulikia miradi ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Vile vile Waziri Jafo kupitia Serikali na Bw. Da Silva kupitia UNOPS wamekubaliana kwamba taasisi hiyo itasadia katika kuchagiza upatikanaji wa fedha kwa wakati za miradi ya maji na umeme zinazotolewa na Benki ya Dunia (WB).

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *