Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akizungumza wakati wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira walipowasili mkoani Ruvuma kwa ajili ya ziara ya kukagua Mradi wa Hifadhi Endelevu ya Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa (SLM-Nyasa) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, leo Machi 16, 2024.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Jackson Kiswaga (katika) akizungumza mara baada ya kamati yake na viongozi mbalimbali kuwasili mkoani Ruvuma kuanza ziara ya Mradi wa Hifadhi Endelevu ya Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa (SLM-Nyasa) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa leo Machi 16, 2024.Kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis na Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira pamoja na wataalamu wakiwa katika kikao wakati wajumbe hao walipowasili mkoani Ruvuma kwa ajili ya ziara ya kutembelea na kukagua Mradi wa Hifadhi Endelevu ya Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa (SLM-Nyasa) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, leo Machi 16, 2024. 

=============================================================================

Serikali imesema imeanza mchakato wa kuangalia namna ya kupunguza kodi katika nishati safi ya kupikia hususan ya gesi ili kushusha gharama za ununuzi kumuwezesha kila mwananchi kumudu kuitumia.

Mchakato huo ni kuhakikisha azma ya Serikali kuwa ifikapo mwaka 2030 wanawake wa Kitanzania na Afrika kwa ujumla wanaanza kutumia jishati safi ya kupikia na kuachana na kuni na mkaa.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema hayo wakati wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira walipowasili mkoani Ruvuma kwa ajili ya ziara ya kikazi leo Machi 16, 2024.

Mhe. Khamis amewahamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia ili kupunguza kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa hatua itakayosaidia kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Halikadhalika, amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais ilianzisha na inaendelea kusimamia kampeni mbalimbali za upandaji wa miti ili kunusuru nchi na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ameitaja Kampeni ya ‘Soma na Mti‘ kuwa inawahamasisha wananfunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo kushiriki kikamilifu katika zoezi la upandaji wa miti kwa wingi.

“Mtakumbuka kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alisisitiza ajenda ya kupanda miti iwe ya kitaifa, hivyo nasi hatuna budi kuisimamia na kuitekeleza ipasavyo,” amesema Mhe. Khamis.

Hivyo, ametoa wito kuwa shughuli zote zinazohusisha viongozi ziambatane na zoezi la upandaji wa miti hatua itakayosaidia kwepo na miti kwa wingi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa kuhitimisha, Naibu Waziri Khamis ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma ambao umebarikiwa kuwa na vyanzo vingi vya maji kuvitunza ili viwanufaishe.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Jackson Kiswaga, inatarajia kutembelea na kukagua utekelezaji wa Mradi wa Hifadhi Endelevu ya Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa (SLM-Nyasa) unaotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa mkoani humo. 

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *