Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akioneshwa jiko linalotumia nishati safi ya kupikia na Mkurugenzi wa Shirika la UpEnergy Tanzania Bi. Rehema Mbalamwezi mara baada ya kufanya mazungumzo kuhusu nia ya shirika hilo katika kuunga mkono Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la UpEnergy Tanzania Bi. Rehema Mbalamwezi (kushoto) mara baada ya kufanya mazungumza kuhusu nia ya shirika hilo katika kuunga mkono Serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam. Kulia ni Meneja kutoa UpEnerg Tanzania Bi. Jacqueline Ngulla.

============================================================================

Serikali imetoa wito kwa mashirika na wadau mbalimbali wa mazingira kuwekeza katika nishati safi ya kupikia ili kurahisisha upatikanaji wa nishati hiyo kwa wananchi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito huo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Shirika la UpEnergy Tanzania Bi. Rehema Mbalamwezi katika Ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam leo.

Katika mazungumzo hayo amempongeza mkurugenzi wa shirika hilo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha jamii kutumia nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuhifadhi mazingira.

Dkt. Jafo amesema kuwa mchango wa shirika hilo wa kuleta majiko yanayotumia nishati safi ya kupikia utasaidia katika kuhamasisha jamii kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia nishati safi

Kutokana na hatua hiyo amelishauri shirika hilo kutanua wigo wa uwekezaji wa nishati hiyo kwa kufungua matawi katika maeneo mbalimbali nchini ili wananchi waweze kufaidika na majiko hayo kwa urahisi na kwa bei nafuu.

Pia, Waziri Dkt. Jafo ameelezea nia ya Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo jambo hilo hivi sasa limeshika kasi likisimamiwa moja kwa moja na Ofisi ya Makamu wa Rais. 

Hivyo, amewataka wawekezaji hao kujitokeza kwa wingi katika kuunga mkono jitihada hizo za Serikali katika kukabiliana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa UpEnergy Bi. Rehema ameelezea adhma ya kampuni hiyo katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikabili nchi na dunia kwa ujumla.

Hivyo, amesema kuwa shirika hilo limekuja na majiko banifu yanayotumia nishati safi ya umeme isiyozalisha gesi joto pamoja na majiko yanayotumia mkaa kidogo. 

Takriban hekta 469,420 za misitu hupotea kila mwaka kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa hali inayosababisha uharibifu mazingira.

Inaelezwa kuwa wanawake ndio waathirika wakubwa wa matumizi ya nishati isiyo safi (kuni na mkaa) hali inayosababisha wakabiliwe na changamoto za kiafya kutokana na moshi unaotoka wakati wanafanya shughuli za upishi.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *